
Faru dume wanaoishi ndani ya Bonde la Ngorongoro mkoani Arusha wapo
katika hatari ya kujeruhiwa au kuuawa na mtoto wa faru John aitwaye
Telele.
Mmoja wa wahifadhi (jina tunalihifadhi) wa faru katika Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), alisema faru huyo amerithi tabia za baba
yake za ukorofi, na tayari ni tishio kwa wenzake.
Faru John aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Agosti 21, mwaka jana
kutokana na uzee na maradhi, anatajwa kuwa mbabe kiasi cha kuwafukuza
faru wengine kutoka Bonde la Ngorongoro na kuua wengine wawili kwa
nyakati tofauti.
Kifo cha faru John kilizua utata mkubwa, kiasi cha Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa, kuagiza ufanyike uchunguzi wa kina ambao bado unaendelea.
Kwa mujibu wa mhifadhi huyo, ubabe wa faru John ulifikia hatua ya
kupigana na baba yake aitwaye Rajabu kuanzia mwaka 2000 na baada ya
vipigo mfululizo, Rajabu alihama kutoka Ngorongoro na kwenda eneo la
Moru katika Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kunusuru maisha yake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo Ngorongoro, faru John anatajwa kuwa faru
mwenye umbo kubwa kuliko faru yoyote barani Afrika na mtoto wake Telele
amechukua umbo la baba yake.
“Baada ya Rajabu kukimbia na kwenda Moru, Serengeti, walibaki madume
watatu ambao ni John, Mikidadi na Runyoro, lakini kadri siku zilivyokuwa
zikienda na ugomvi ulikuwa ukizidi, kila mmoja akitaka kuwa mkuu wa
himaya, huku madume mengine yakiendelea kukua.
“Madume hayo ni pamoja na Msekwa, Telele, Ndugai na Selelii, na huyu Telele ana umbo kama la John na mkorofi sana.
“Mwaka 2003 mapigano yalizidi hadi pembe ya John ikakatika katika
mojawapo ya matukio hayo ya kupigana, na baadaye Mikidadi na Runyoro nao
walilazimika kukimbia, lakini baada ya kukatika, pembe hiyo ilianza
kuota tena na kurudi kwenye makali yake.
“Baada ya madume hayo mawili kukimbia, mwaka 2012 faru John alimjeruhi
kwa pembe mtoto wake mwingine aitwaye Cheusi… pembe ilipenya na kumchoma
kwenye mapafu na maini na kumsababishia madhara makubwa,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo Ngorongoro, mwaka 2014 ilibidi pembe ya
John ikatwe na mtaalamu kutoka Afrika Kusini, Peter Morkel, ambaye baada
ya kuikata aliweka kifaa maalumu cha utambuzi (transmitter), ambacho
kipo ndani ya mojawapo ya pembe alizokabidhiwa Waziri Mkuu Majaliwa
usiku wa kuamkia Desemba 8, mwaka jana.
“Kuna wakati vikao vilipendekeza John apelekwe Afrika Kusini, lakini
kutokana na historia yake ya ugomvi, wenzetu wa kule walikataa,” alisema
mtoa taarifa.
TABIA NA MAISHA YA FARU
Kwa mujibu wa wahifadhi wa faru waliopo Ngorongoro na Serengeti, faru
dume wana tabia ya kupigana kila mmoja akitaka kuwa mtawala wa wengine.
Mapigano ya faru wakati mwingine hudumu hata kwa zaidi ya saa tano na yanaweza kusababisha majeraha makubwa na hata kifo.
Ili kuwaachanisha faru wanaopigana, inabidi itafutwe gari na kuingia
kati yao, na kwa kawaida baada ya kazi ya kuwaachanisha, gari huharibiwa
vibaya na faru hao.
Pia faru jike akishapandwa, huchukua miezi 18 kuzaa, na kutokana na
mazingira asilia mazuri kwa faru katika Bonde la Ngorongoro, anaweza
kubeba mimba miezi sita baada ya kuzaa.
Hivi sasa kuna faru zaidi ya 50 Ngorongoro, kutoka faru 10 katika miaka
ya 1980 hadi 1990, jambo linalotajwa kuwa limelotokana na juhudi kubwa
na umakini katika uhifadhi wa mnyama huyo.
COMMENT AND SHARE....................!!!!!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!