Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo, Mifugo na
Uvuvi kuhakikisha inafufua sekta ya ushirika na kuwachukulia hatua kali
watendaji wote waliohujumu ushirika na kusababisha machungu kwa
wanaushirika ili iwe fundisho kwa wengine.
Pia ameitaka wizara hiyo kupitia upya sekta ya ushirika kwa kuanza na
viongozi walipo ndani ya wizara hadi mikoani kuhakikisha kama wanafanya
kazi zao ipasavyo na kuwaondoa watakaobainika kwa uzembe.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati akifunga maadhimisho ya
Sherehe za Wakulima Nanenane kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,
yaliyofanyika kwenye Uwanja wa John Mwakangale mkoani Mbeya.
Alisema mkulima, mfugaji na mvuvi mdogo au mmoja mmoja hawezi
kupunguza umasikini bila ya kuwa na chombo cha kuwaunganisha na kuwapa
nguvu ya kutetea bei ya mazao yao kama ushirika. Aidha alisema ushirika
imara utawasaidia kutafuta soko na kupata mikopo ya riba nafuu.
Alisema pamoja na umuhimu wa kuwepo kwa ushirika, tasnia hiyo
imewaumiza wakulima wengi na kuwafanya kukata tamaa katika uzalishaji
kutokana na usimamizi mbovu, ubadhirifu na ubabe wa baadhi ya viongozi
wa ushirika.
“Wahimizeni na kuwashawishi wakulima, wafugaji na wavuvi kujiunga
katika vikundi vya ushirika vya uzalishaji na Saccos. Aidha, elimu ya
ushirika inayotolewa kwenye maonesho ya mwaka huu, iwe changamoto kwenu
kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,” alisema.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema Serikali haitamvumilia mfugaji
anayelisha katika maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji na aliwataka
wakuu wa mikoa na wilaya waendelee kulinda maeneo hayo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole
Nasha alisema sekta ya kilimo imekuwa na mafanikio makubwa ambapo katika
kipindi cha miaka minne mfululizo nchi imeweza kuzalisha chakula cha
ziada, ambapo kwa mwaka huu imezalisha kwa asilimia 123.
“Mafanikio hayo yanachangiwa na jitihada za Serikali katika kutoa
ruzuku ya pembejeo, taasisi za utafiti ambazo zimekuwa zikitafiti aina
bora ya mbegu zikitafuta mbegu bora na wakulima walioamua kuwekeza
kwenye kilimo,” alisema.
Naibu Waziri Ole Nasha alisema katika ukanda wa Nchi za Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni nchi mbili tu za Tanzania na
Zambia kati ya nchi 15 za jumuiya hiyo, hazikabiliwi na baa la njaa.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata)
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ladislaus Mwanakatwe aliipongeza Serikali
kwa jitihada zake za kuwatetea pamoja na utatuzi wa kero za muda mrefu
zilizokuwa zinawakabili wakulima ikiwemo ya tozo.
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!