Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi
wasikilizaji na karibuni katika kipindi chenu chenye faida tele cha
Ijue Afya Yako. Leo tutazungumzia tatizo la maambukizi katika njia ya
mkojo Urinary Tract Infection ugonjwa ambao unawasumbua sana wanawake
wengi na watoto katika nchi nyingi zinzoendelea.
&&&&&&
Maambukizi katika njia ya mkojo au
kama unavyojulikana kwa wengi UTI huathiri mfumo wa mkojo ikiwa ni
pamoja na ureter ambayo ni kama bomba linalosafirisha mkojo kutoka
kwenye figo, pia kibofu cha mkojo na urethra. Ugonjwa huu unaathiri
zaidi kibofu cha mkojo na urethra lakini unaweza pia kuathiri figo.
Maambukizi haya yakiathiri sehemu za chini za kibofu cha mkojo kitaalamu
huitwa simple cystitis au Bladder infection, na maambukizi hayo
yakitokea sehemu za juu za mfumo wa mkojo huitwa pylonephritis au kidney
infection. Ugonjwa huu husababishwa na bakteria anayeitwa Escherichia
coli (E. coli) na tatizo hili husababishwa kwa kiasi kikubwa na bakteria
ambao makazi yao ya kawaida ni kwenye utumbo mpana, na hivyo huwa
wanapatikana pia kwenye haja kubwa. Lakini baadhi ya watu wanaweza
kupata tatizo hili kutokana na kuingiwa na fangasi ingawa pia zipo
sababu nyingine chache. Bakteria wa Escherichia coli hawasababishi peke
yao UTI bali huambatana na wengine waitwao staphylococcus, saprophyti
cus, pseudom onas, enterobacter na kadhalika. Maambukizi katika njia ya
mkojo lazima yawe ni kwenye njia ya mkojo na si pengine popote. Wapo
wanawake ambao wamekuwa wakidhani kwamba tatizo la kutokwa na uchafu
ukeni ni ugonjwa huu, na hilo si sawa kwani huo ni ugonjwa tofauti
kabisa na UTI. Tunapozungumzia maambukizi katika njia ya mkojo,
inamaanisha ni kutoka eneo la nje ya utupu hadi kwenye kibofu na kutoka
kwenye kibofu hadi kwenye figo. Kama maambukizi yako katika eneo la
kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo, kitaalamu huitwa Lower Urinary
Tract Infection na yakihusisha eneo la juu ya kibofu jina hubadilika na
kuitwa, Upper Urinary Tract Infection. Mara nyingi maambukizi haya kwa
wanawake husababishwa na kutojisafisha vizuri sehemu za siri na kuvaa
nguo za ndani zilizochafu. Pia huweza kusababishwa na matumizi ya pedi
za kike zenye kemikali ya kukata harufu ambazo huua bakteria wa asili wa
eneo la uke na kuwapa fursa bakteria wanaosababisha maradhi kuzaliana
kwa wingi. Halikadhalika upungufu wa homoni ya wanawake iitwayo
Oestrogen husababisha bakteria wanaosababisha maambukizi katika njia ya
mkojo kuzaliana kirahisi. Matumizi ya baadhi ya dawa kwa muda mrefu,
unywaji wa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu na kutokunywa maji ya
kutosha pia huchangia tatizo hili. Uwepo wa mawe katika figo na mirija
ya figo pia ni mojawapo ya chanzo cha maambukizi haya katika njia ya
mkojo. Sababu nyingine inayosababisha UTI ni matumizi ya maji machafu
wakati wa kujisafisha au kuoga ambayo huweza kuweka bakteria kwa urahisi
na kupelekea mwanamke kupata ugonjwa huo. Uchafu wa vyoo umetajwa kuwa
sababu nyingine, kwani matumizi ya vyoo ambavyo ni vichafu huweza
kusababisha mwanamke kupata UTI kwa sababu ndani ya choo kuna bakteria
wengi ambao wanaweza kusababisha ugonjwa huo.
&&&&&&
Matatizo haya ya maambukizi licha ya
kuwapata zaidi wanawake, huwakumba pia watoto wadogo wa kike kutokana
na sababu za kimaumbile ambapo viungo vyao vya uzazi, njia ya mkojo na
haja kubwa vipo jirani. Watoto wa kiume ambao hawajatahiriwa nao huweza
kupata maambukizi rahisi ya UTI iwapo watajisafisha kwa kutumia maji
yasiyo salama ambapo huwa rahisi kwa bakteria kubaki katika ngozi
inayoning'inia (govi). Pia wanaume watu wazima ambao hawajatahiriwa
wanaweza kupata maambuzi ya UTI kutokana na sababu tuliyoitaja ambapo
pia ni rahisi kwao kuambukizwa Ukimwi kama watafanya ngono zembe na
ndiyo maana tohara kwa wanaume husisitizwa.
Maambukizi
yanayoshambulia mfumo wa mkojo husababishwa zaidi na bakteria wanaoishi
katika mfumo wa haja kubwa kwa kuingia na kujikita katika mfumo wa
mkojo. Bakteria wengine wanaoleta maabukizo katika njia ya mkojo ni wale
watokanao na magonjwa ya zinaa kama kisonono, klamidia, trimonas na
fangasi ambapo huwaathiri watu pale wanapojamiiana bila kutumia kinga na
watu wenye maradhi hayo. Ili kuepuka kupata maambukizi katika njia ya
mkojo, mara kwa mara, ni vyema kutumia kinga na kwa mwanamke wanashauri
kila wanapomaliza kufanya tendo la ndoa wakojoe ili kuondoa bakteria
walioingia au waliokaa katika tundu ya mkojo wakisubiri kuingia. Baada
ya kujua hayo yote hivi sasa tuzijadili dalili za ugonjwa wa UTI.
Baadhi
ya dalili za mtu kuambukizwa bakteria katika njia ya mkojo kubwa ni
maumivu wakati wa kukojoa, mkojo kuwa na rangi ya njano kupindukia na
kuwa na harufu kali ijapokuwa siyo kila mwenye dalili hizo ana
maambukizi katika njia ya mkojo. Dalili nyingine za UTI ni maumivu,
kutokwa na usaha wakati wa kukojoa, kabla au baada ya kukojoa
kukiambatana na maumivu na kuhisi moto wakati mkojo ukitoka. Baadhi ya
wanaume wakati mwingine hutokwa na majimaji katika njia ya mkojo wakati
wa kujisaidia haja kubwa. Wengine wenye maambukizi hujikuta wakipata
vichomi katika njia ya mkojo, au kuhisi kuwashwa sehemu hiyo, kuumwa
kiuno au tumbo na kadhalika. Mgonjwa anaweza pia kukumbwa na homa kali
mara kwa mara na mwili kuwa mchovu, kwa watoto hupoteza hamu ya kula na
mwili huonesha kuchoka.
Wagonjwa wengine hupata maumivu kwenye kibofu
cha mkojo ambapo husikia maumivu ya chini ya tumbo usawa wa kitovu na
huwa hayaishi. Matatizo haya ya mfumo wa mkojo kama tulivyoona kabla
huwapata watu wote wanawake na wanaume. Watu wenye matatizo haya kila
wakipima huambiwa wana UTI. Kwa wanaume huhisi hata nguvu za kiume
kupungua na wanawake hupoteza hamu ya tendo la ndoa.
Kwa wajawazito
ugonjwa unaweza kuhatarisha maisha yao na mtoto aliye tumboni. Bakteria
wanaweza kuingilia mfumo wa damu na kusababisha madhara mengine kama
vile shinikizo la damu kuwa kubwa kwenye figo na hata kusababisha
ufanyaji kazi mbovu wa figo.
&&&&&
Maambukizi katika njia ya mkojo
hutibika kwa dawa mbalimbali za kisasa baada ya kufanyiwa vipimo na
kuthibitika kuwa mgonjwa ana maambukizi hayo. Dawa ambazo anaweza kupewa
ni kama vile Ciprofloxacin, Monurol, Furadantin, Sulfam ethoxazole,
co-trimax, ampicillin, gentamicin na kadhalika. Mgonjwa anayesumbuliwa
na UTI hapaswi kutumia dawa yoyote bila kwanza kupata ushauri wa
daktari.
Wanawake wanashauriwa kuepuka kujisafisha sehemu za siri na
maji machafu na yasiyo salama, pia kuepeuka kupaka marashi sehemu hizo,
ama kutumia pamba zenye kemikali ya kukata harufu kwani hizo huua
bakteria wa asili wa ukeni hali ambayo hukaribisha bakteria wa maradhi
kuzaliana kwa wingi. Pia wanashauriwa wanapojisafisha baada ya
kujisaidia kuanzia mbele kwenda nyuma, ili kuepusha kuhamisha bakteria
walio eneo la haja kubwa na kuingia njia ya mkojo. Kwa wale walio katika
kipindi cha ukomo wa hedhi, wanaweza kushauriana na daktari juu ya
kutumia oestrogen ya ukeni ili kuwasaidia kujikinga na maambukizi ya
UTI. Kwa mwanaume maambukizi haya huathiri nguvu za kiume na kujipenyeza
hadi katika korodani na huathiri uzalishaji wa mbegu za kiume na
kunaweza hata kusababisha mgumba. Hivyo wanashauriwa kuhakikisha
wanatibu bila kuchelewa ugonjw ahuo. Pia maambukizi ya njia ya mkojo
huweza kusababisha matatizo ya tezi ya kiume (prostate) kwani
husababisha mrija wa mkojo kuziba, kutopitisha mkojo vizuri na kuruhusu
bakteria kujenga makazi. Hali hiyo ikitokea mgonjwa lazima akamuone
daktari ili awekewe mrija wa kutolea mkojo.
Mpenzi msikilizaji
madaktari wanatueleza kuwa, tunaweza kuudhibiti au kuponya ugonjwa huu
kwa kunywa maji mengi pamoja na juisi itokanayo na matunda halisi, iwapo
tutawahi kabla tatizo halijawa sugu. Kwa maana nyingine, unaweza
kujikinga na ugonjwa huu kwa kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha
kila siku. Ukinywa maji ya kutosha yatakufanya uende haja ndogo kila
mara na kwa njia hiyo wale bakteria watakuwa wakitoka na hatimaye kuisha
kabisa. Katika hali ya kawaida, ugonjwa wa UTI hutoweka ndani ya siku
tatu mara baada ya kuanza kutumia tiba asili ya kunywa maji mengi na
juisi ya matunda halisi, iwapo ugonjwa utaendelea kuwepo baada ya siku
hizo, hiyo itakuwa na maana ugonjwa wako umeshakomaa na hivyo hauwezi
kutibika kwa tiba hii ya nyumbani na itakuwa inapaswa kwenda hospitalini
na kuonana na daktari ambaye atafanya uchunguzi na kutoa dozi sahihi ya
kutibu ugonjwa huo.
Wasikilizaji wapenzi tutaendelea kujadili
ugonjwa wa maambukizo katika njia ya mkojo kwenye kipindi chetu kijacho.
Hadi wakati huo tusisahau kuzilinda afya zetu na kwaherini.
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!