TANZANIA iko kwenye hatua za kuridhisha katika utafiti wa miti maalumu
inayoaminika itakuwa chanzo cha dawa maalumu ya kuzuia na kutibu maradhi
sugu ya tezi dume pamoja na saratani ya kibofu, matatizo yanayowasibu
wanaume wengi duniani.
Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo eneo la
Tengeru wilayani Meru mkoani hapa, inafanyia utafiti mti mwekundu wa
asili ujulikanao kama ‘kiburabura,’ unaopatikana katika msitu wa Magamba
wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Ingawa katika hali ya kawaida utomvu wa mti huo wa kiburabura
(unaojulikana kisayansi kama Prunus Africana) unadaiwa kuwa ni sumu,
lakini wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha
Nelson Mandela wanasema hilo hasa ndilo litakuwa chimbuko la tiba ya
uhakika kwa matatizo ya tezi dume, saratani ya kibofu na magonjwa
mengine ya viungo vya uzazi.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Nelson Mandela, Dk Mussa Chacha alisema mjini
hapa kuwa, utafiti huo wa miti hiyo ya asili kwa ajili ya tiba, ulianza
miezi sita iliyopita na kwamba upo katika hatua nzuri, ingawa hakusema
kuwa watakamilisha lini mradi huo ili kuifanya Tanzania kuingia kwenye
historia ya dunia kama wavumbuzi wa tiba ya maradhi hayo yanayowasumbua
wanaume wengi duniani na hata kusababisha vifo.
Alikuwa akitoa maelezo ya chuo hicho cha Nelson Mandela kwa Waziri wa
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako aliyekuwa anazitembelea taasisi kadhaa za sayansi na
teknolojia mkoani hapa, kikiwemo Chuo cha Nelson Mandela (NM-AIST) na
Tume ya Mionzi (TAEC).
“Kutokana na uharibifu wa mazingira na miti kukatwa hovyo, hivi sasa mti
huu wa kiburabura umeanza kutoweka nchini, lakini kuna baadhi ya mimea
hii ambayo inapatikana katika msitu wa Magamba wilayani Lushoto na
tayari wenyeji wa eneo hilo wanakiri kutumia magamba ya mti huo kwa
ajili ya tiba za malaria na matatizo ya viungo vya uzazi,” alisema
mkufunzi huyo.
Zaidi ya wanaume 30,000 hufa kila mwaka kutokana na matatizo ya saratani
ya kibofu. Ugonjwa huu mara nyingi huwapata watu wazima kuanzia umri wa
miaka 45 na kuendelea.
Sasa wasomi wa Tanzania wako mbioni kugundua dawa ya moja kwa moja.
Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo kwa
wanaume duniani.
Pia ni chanzo kikuu cha vifo kwa wanaume wenye umri wa miaka 70 na kuendelea.
Tafiti za Chama cha Saratani cha Marekani (ACS) na cha Afrika Kusini
(CANSA) zimebaini kuwa, mwanamume mmoja kati ya sita hupata saratani ya
tezi dume katika uhai wake.
Kutokana na takwimu za mwaka 2010 za dunia nzima, malaria iliua watu
500,000, kifua kikuu watu milioni 2.1, Ukimwi watu milioni 1.8 na
saratani watu milioni 9.9.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na
ugonjwa wa saratani ni kubwa ikilinganishwa na ya magonjwa mengine.
Dk Emmanuel Kandusi ambaye ni miongoni mwa waathirika wa saratani hiyo,
na mwanzilishi wa kampeni ya kuangamiza saratani ya tezi dume Tanzania
ya ‘50 Plus Campaign’ anasema ugonjwa huo ukitambuliwa mapema huweza
kutibika kwa urahisi.
Ameongeza kuwa kutokana na ugonjwa huo kuwa hatari nchini humo, ifikapo
mwaka 2020 unatarajiwa kuua watu milioni 20. Matibabu ya ugonjwa huo ni
pamoja na kupata dawa pamoja na upasuaji.
Naye Profesa Ndalichako alisifu jitihada za Nelson Mandela katika
kufanya tafiti zenye tija na kuongeza kuwa serikali imetenga zaidi ya Sh
bilioni 8.3 kwa ajili ya maendeleo ya elimu katika taasisi hiyo ikiwemo
vifaa vya maabara na utafiti pamoja na udahili wa wanafunzi.
Fedha hizo zikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Wakati huo huo, utafiti wa Taasisi ya Africa Capacity Building
Foundation kwa mwaka huu unaonesha kuwa Tanzania iko katika nafasi ya
pili barani Afrika katika matumizi ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya
kujiletea maendeleo.
COMMENT AND SHARE......................!!!!!!!!!!!!
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!