
Wengi wamejikuta wakiitwa wahuni kutokana na kuwa na uhusiano wa
kimapenzi na makundi ya wanaume au wanawake. Hata hivyo wachunguzi wa
masuala ya mapenzi wanasema idadi kubwa ya wapenzi si kigezo sahihi cha
kupima tabia ya mtu na kumhusisha na uhuni.
Watalaam hao wanataja safari ya kupata chaguo halisi la
mwanaume/mwanamke wa maisha ndiyo inayowaponza wengi kiasi cha kujikuta
wameingia katika kashfa ya kuwa na uhusiano na dazeni ya wapenzi.
Wanasema msichana/mvulana anayeingia katika uwanja wa mapenzi kwa kuwa
na hisia za kufanya ngono, hukosa umakini wa nani anafaa kuwa mpenzi
wake kutokana na kukosa elimu ya uhusiano kutoka kwa wazazi wake.
Kwa mantiki hiyo, bila upembuzi wa kina, mtu asiye na elimu ya jinsi ya
kumpata mpenzi wa kweli hujikuta ameangukia kwa mwanaume/mwanamke
asiyemfaa, ambapo baadaye huamua kuachana na huyo na kwenda kwa mwingine
kujaribu bahati tena ya kupata penzi la kweli.
Zinatajwa zawadi, hitaji la kusaidiwa kimaisha, mvuto wa kimahaba na
mazoea kuwa ni vichocheo vinavyowaangusha wengi kwenye mapenzi na
wasiowafaa.
Ukweli ni kwamba mtu aliyenaswa kwa ‘ujinga’, huwa hakatwi kiu ya penzi
na mwanaume/mwanamke asiye chaguo sahihi la maisha yake. Hivyo hufikia
maamuzi ya kujiingiza katika uhusiano mpya mara 2,3,4,5 na kujikuta
wakiambulia wanaume/wanawake wale wale wasio sahihi kwake.
Mwanamnke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Suzzy aliwahi kuniomba
ushauri, akasema amechoka kuchezewa, maana kila mwanaume anayempata
anakuwa si chaguo lake. Lakini kibaya zaidi kuachia ngazi au kutemwa
huku akiwa tayari ameshafanya mapenzi na wanaume hao.
Nia ya swali lake ilikuwa ni kuniomba njia za kumtambua mwanaume mkweli
bila kufanya naye mapenzi? Aliuliza hivyo huku akiwa na hoja kuwa
wanaume wengi hawako tayari kuwa na uhusiano na msichana bila kufanya
naye mapenzi na wakati huo huo huficha tabia zao chafu wakilenga kumnasa
wamtakaye.
Binafsi nafahamu kuwa kuna wanawake/wanawake wengi ambao hujiingiza
katika mapenzi kwa kutekwa na hadaa za mwili na kujikuta wanacheza
mchezo wa kitoto wa pata potea.
Ni madhumuni ya somo hili kufundisha vigezo vya kumpata
mwanaume/mwanamke halisi wa maisha, bila kufanya naye mapenzi. Njia hii
ina faida kwa pande zote mbili yaani kwa mwanamke na mwanaume kwani
kuacha au kuachwa bila kufanya mapenzi ni bora kuliko kuwa muonjaji,
tabia ambayo huathiri kisaikolojia na ni hatari kwa afya.
Ifuatavyo ni njia ya kisaikolojia ambayo mwanamke anaweza kutumia
kumpata mwanaume mwenye kumfaa bila kufanya naye mapenzi tena ni jibu
sahihi la kuondokana na mchezo wa kubahatisha kwa wanaume wanaosaka
wapenzi wa kweli na si taksi bubu ambazo mchana huweka namba za njano
usiku nyeusi.
KWANZA- Ni ya mwanamke/mwanaume mwenyewe kujifahamu na kufahamu vigezo
vya mpenzi anayemhitaji katika maisha yake. Ifahamike kuwa kila mwanaume
ana wake na kila mwanamke anaye wake wa maisha pia. Hivyo asiyekufaa
wewe anawafaa wengine, kinachotakiwa ni wewe kujitambua kwanza ili
umtambue umtakaye.
Wanawake/wanaume wengi hawafahamu wanahitaji wapenzi wa aina gani, hivyo
wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni bila kujua wanataka kununua
nini? Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli wa mapenzi, wakachezewe
na kuumizwa moyo bure.
PILI- Ni kuketi chini na kuorodhesha vigezo stahili vya
mwanaume/mwanamke unayemtaka. Baada ya hapo orodhesha tena kasoro za
mwanaume/mwanamke unazoweza kuzivumilia na zile ambazo huwezi
kuzivumilia kabisa. Hii inatokana na ukweli kwamba mwanadamu
hajakamilika, ana upungufu wake.
TATU- Anza kumsaka kwa kutumia milango ya fahamu. Cha kufanya hapa ni
kuruhusu macho yawaone wanaume/wanawake na kuwatathmini kwa maumbile yao
ya nje na kisha kupata majibu kutoka moyoni juu ya kuvutia kwao ambako
hutambulika kwa moyo kurithika na mwili kusisimka.
NNE - Kuanzisha safari ya kuchunguza tabia za nje na za ndani kivitendo.
Hapa suala la ukaribu baina ya mwanaume na mwanamke linahitajika.
Msingi unaotajwa hapa ni kujenga mazoea ya kawaida yasiyokuwa na masuala
ya kimapenzi na ngono. Kutambuana, dini, viwango vya elimu, kabila na
makundi ya marafiki ni mambo ya kuzingatia.
Katika uchunguzi huu mwanamke/mwanaume anayetafuta mpenzi hana budi
kupitia na kumlinganisha huyo aliyempata na vigezo alivyojiwekea. Zoezi
hili liendane na kuweka alama ya pata kila anapobaini kuwa
mwanaume/mwanamke anayemchunguza amepata moja ya vigezo vyake. Lakini
pia aweke alama ya kosa kwa kila kasoro anayoivumilia na ile
asiyoivumilia.
TANO - Ajipe muda wa kutosha kati ya miezi sita na mwaka kumchunguza
huyo mwanaume, kisha aketi chini na aanze kujumlisha alama za vigezo
alivyovijiwekea na jinsi mwanaume huyo alivyopata au kukosa.
Ikibainika mwanaume aliyechaguliwa amepata zaidi ya nusu ya alama ya
vigezo vilivyowekwa, basi ujue kuwa anafaa. Kuhusu alama chache
alizikosa anaweza kusaidia kuzikamilisha polepole wakati wa maisha ya
ndoa.
Lakini angalizo kubwa kabisa ni kwamba mwanaume/mwanamke akionekana
kuanguka katika kasoro zisizoweza kuvumilia kwa zaidi ya alama tatu.
Yaani kwa mfano ni mlevi, mwizi, muongo, mbishi na katika hizo kashindwa
3, huyu hafai, ni vema akawekwa kando kwani huwezi kubeba kero 3 kwa
pamoja katika maisha.
SITA - Kusajili mapenzi yenye malengo yanayotekelezeka. Lazima baada ya
kuchunguzana kwa kina wapenzi watengeneze muongozo wa mapenzi yao.
Wasiwe kama wanyama, lazima mipango ya wapi wametoka walipo na
wanapokwenda.
Hata hivyo watalaam wanasema lazima wapenzi wapime umakini wao kwa
vitendo. Kama wamekubaliana kuoana, suala la mume kwenda kujitambulisha
kwa wakwe na hatua ya kuiendea ndoa ionekane. Usiri usiwepo tena. Kila
mmoja amuone mwenzake kama sehemu ya maisha yake na mara zote wasaidiane
kwa ukaribu.
SABA - Ni vema ndugu wakashirikishwa ili kuwapa nafasi na wao ya kuamua
kama mapenzi hayo ni budi yakaendelea au yakasitishwa. Ni ukweli ulio
wazi kwamba licha ya wengi kupuuza maamuzi ya ndugu kwa madai ya kuwa
hawana nafasi kwa wapenda nao, lakini uchunguzi unaonesha kuwa wapenzi
wengi huacha kutokana na sumu za ndugu hasa pale wanapokuwa wameonesha
kutounga mkono uhusiano wa wanaotaka kuoana
NANE - Hatua hii ni ya kuweza kuzungumzia ufanyaji mapenzi, hapa nina
maana kama wapenzi wamejizuia kwa muda mrefu na wanahisi kuchoka
wanaweza kujadiliana kuhusu hilo na kuamua ufanyaji huo wa mapenzi una
lengo gani, kama ni kuburudisha miili basi suala la afya na uzazi salama
litazamwe.
TISA - Kutimizwa kwa ahadi ya kuoana ni hatua ya tisa ambayo nayo si
busara ikachukua muda mwingi kutekelezeka, kwani ucheleweshaji mwingi wa
ndoa nao huvunja moyo na mara nyingine umewafanya wengi kutoaminiana.
KUMI - Kuamua kuwa mwili mmoja kwa kuvumilia na kuwa tayari kukabiliana
na changamoto zote za maisha ukiwemo mkwamo na dhiki ambazo huchangia
sana ndoa nyingi kuvunjika. Hapa pia ni wajibu wa wanandoa kuchukuliana
udhaifu na kusaidia, kuwa tayari kujifunza na kujali zaidi upendo kuliko
hisia za mwili ambazo wakati mwingine hudanganya na hivyo kumfanya
mwanandoa asivutiwe na mwenzake.
Mwisho ni kwamba kanuni hizi huwafaa watu wazima mapenzi ya kitoto
hayawezi kujenga misingi hii imara mara nyingi ni kudanganyana,
kuharibiana maisha, kupeana mimba na maradhi.
COMMENT AND SHARE................!!!!!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!