BALAA LINGINE MCHANA HUU:.ADA ZA SHULE MUHULA MPYA PASUA KICHWA HII HAIJAWAHI KUTOKEA:;
on
Get link
Facebook
X
Pinterest
Email
Other Apps
NI pasua kichwa! Utaratibu mpya wa kulipa ada katika baadhi ya shule za binafsi nchini unaelekea kuwachanganya wazazi kutokana na ongezeko la kiwango cha malipo huku wamiliki wakidai kuwa hawana namna kwakuwa wanatimiza agizo la Serikali kuhusiana na vipindi vya muhula wa masomo
Uchunguzi wa Nipashe uliohusisha mahojiano na wadau kadhaa wakiwamo
wazazi na wamiliki wa shule, umebaini kuwa agizo la Serikali la kuzitaka
shule zote kuwa na mihula miwili ya masomo na siyo zaidi ya hapo ndilo
linalotumika kama kigezo kwa baadhi ya shule kuwataka wazazi walipe ada
za watoto wao kwa mikupuo miwili tu kwa mwaka ili kuendana na idadi ya
sasa ya mihula kwa kipindi hicho; na siyo kama ilivyokuwa awali ambapo
baadhi waliruhusu wazazi kulipa kwa mikupuo hadi minne kutokana na
utaratibu waliokuwa nao wa mihula.
Matokeo yake, Nipashe imebaini kuwa baadhi ya wazazi wamejikuta katika
wakati mgumu kwa sasa, sababu ikiwa ni kuwapo kwa ongezeko la hadi mara
mbili ya kiwango cha fedha wanachotakiwa kuwalipia watoto wao.
Hata hivyo, uchunguzi wa Nipashe umebaini vilevile kuwa baadhi ya shule
zimelazimika kuwasikiliza wazazi kwa kuruhusu waendelee kulipa kwa
mikupuo zaidi ya mwili, lengo likiwa ni kuwapa fursa ya kuzoea utaratibu
huo mpya unaoendana na idadi ya mihula.
Nipashe ilibaini kuwa katika baadhi ya shule ambazo ada yake ni Sh.
milioni tatu kwa mwaka, ulipaji wa mikupuo minne ulikuwa Sh. 750,000 kwa
muhula, lakini sasa kutakuwa na malipo ya mikupuo miwili ambayo mzazi
atalazimika kulipa Sh. 1,500,000 kwa muhula.
Aidha, kwa shule ambayo ada yake ni Sh. milioni mbili kwa mwaka, ulipaji
wa mikupuo minne ya zamani ulikuwa Sh. 500,000 kwa muhula, lakini kwa
mihula miwili ya sasa, mzazi hulazimika kulipa Sh. milioni moja kila
muhula.
Baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, pamoja na mambo mengine, Prof. Joyce
Ndalichako, alitangaza uamuzi wa Serikali wa kupiga marufuku utaratibu
wa baadhi ya shule wa kuwa na mihula zaidi ya miwili kwa mwaka mmoja wa
masomo.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, baadhi ya wazazi wenye
watoto wanaosoma shule za msingi binafsi walisema utaratibu wa sasa
unawapa wakati mgumu kwa sababu hali ya kifedha imekuwa ngumu na zaidi
ya yote, walishajiandaa kitambo kuwalipia ada watoto wao kwa utataribu
wa awali wenye mikupuo zaidi ya miwili.
“Mimi nina watoto watatu, na kwa wastani kila mtoto huwa namlipia ada ya
Sh. 500,000 kwa kila mkupuo katika awamu tatu kwa mwaka… sasa naambiwa
nilipe Sh. 750,000 kwa kila mtoto kwa sababu ni lazima nimalize kwa
awamu mbili, nitaziotoa wapi? Sikuwa nimejiandaa kwa mabadiliko hayo,”
alisema mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Mama Halima, mkazi wa
Kijitonyama.
Magreth Mshana, mmoja wa wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule
binafsi iliyopo jijini Dar es Salam, alisema ada kulipwa katika mihula
miwili inawezekana, lakini kuna changamoto ya wamiliki wa shule hizo
kupandisha ada kiholela bila kujali ubora wa huduma inayotolewa na shule
husika na hivyo ni bora Serikali ikaingilia kati kwa kutoa ada elekezi
kama inavyofanya katika kusimamia mafuta na nishati.
WAMILIKI WA SHULE
Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki na
Mameneja wa Vyuo na Shule Binafsi Tanzania (Tamongsco), Benjamin Nkonya,
alisema ulipaji wa ada katika shule hizo kwa awamu mbili umetokana na
utekelezaji wa tamko la serikali na hivyo wazazi na walezi wa wanafunzi
hawana namna nyingine isipokuwa ni kujipanga upya kwa utekelezaji.
Alisema njia mojawapo ya kufanikisha jambo hilo ili hatimaye watoto wao
waendelee kupata elimu bora ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Alisema katika serikali ya sasa ya awamu ya tano, wazazi wanatakiwa
kufuata na kuunga mkono kauli ya kubana matumizi kwa vitendo, ikiwa ni
pamoja na kuacha kutumia fedha katika matumizi yasiyo ya lazima na
badala yake waelekeze nguvu katika shughuli za maendeleo ikiwamo elimu
ya watoto wao.
“Wazazi, walezi wapunguze starehe. Michango isiyo ya lazima kama harusi,
mtu anachangia hadi laki (Sh. 100,000) au milioni kufanikisha tukio la
siku moja tu, hapo hapo ukimwambia ada ilipwe kwa awamu mbili, anaona
mzigo. Ukweli ni kwamba wabane matumizi, waache kushinda baa,” alisema
Nkonya.
Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Lord Baden Powell
iliyopo Bagamoyo, Kanali Mstaafu Idd Kipingu, alisema ada kwa mwaka
shuleni kwake inalipwa kwa awamu mbili, ingawa wametoa fursa kwa mzazi
au mlezi anayeshindwa kulipa kwa awamu hizo mbili, kulipa mara tatu.
“Inalipwa kwa awamu mbili, lakini mzazi akijieleza na kutokana na ugumu
wa fedha katika kipindi cha Januari, atalipa kwa awamu tatu,” alisema
Kipingu.
Agustino Mwalongo, mmoja wa viongozi wa Shule ya Sekondari Barbro
iliyopo jijini Dar es Salaam, alisema ada kwa mwaka kwao hulipwa kwa
awamu mbili kulingana na mwongozo wa serikali wa kuzitaka shule kuwa na
mihula miwili tu kwa mwaka.
Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Winning Spirit iliyopo mkoani Arusha,
Maximillian Iranke, alisema ada katika shule yao inalipwa kwa awamu nne,
ingawa mihula ya masomo ipo miwili kulingana na mwongozo wa serikali.
“Ada inalipwa kwa awamu nne, Januari, Aprili, Julai na Septemba… lakini
mihula ya masomo ni miwili kama serikali inavyosema,” alisema Iranke.
MSISITIZO WA AGIZO LA SERIKALI
Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Kaimu Kamishna wa Elimu, Venance Manori,
alisema wizara hiyo itazifutia usajili shule zote binafsi
zitakazobainika kukiuka agizo hilo la kuzitaka kuwa na mihula miwili ya
masomo kwa mwaka badala ya mitatu hadi minen kwa baadhi yao.
Ili kutekeleza azma hiyo, Manori alisema wizara hiyo iliwaagiza wakaguzi
wa shule pamoja na maofisa elimu wa wilaya, kufanya ukaguzi katika
shule binafsi zilizoko katika maeneo yao; kubaini kama kuna shule
binafsi zilizokaidi kutekeleza Waraka wa Elimu Namba Moja wa Mwaka 2015.
Alisema wizara yake ilitoa waraka huo ikiwa ni njia ya kukazia Waraka wa
Serikali Na. 5 wa Mwaka 2012 ambao ulikuwa unaelekeza mihula ya masomo
kwa shule za sekondari na vyuo vya ualimu, ifanane ili kuepusha usumbufu
kwa walimu na wanafunzi.
Waraka huo ulifafanua kuwa kila muhula utakuwa na likizo fupi na likizo
ya mwisho wa muhula na siku za masomo kwa mwaka zitakuwa ni 194.
Pia waraka huo unataka siku za michezo ya Umitashumita na Umiseta kwa shule za msingi na sekondari, zifanane kwa shule zote.
“Ule waraka ulisambazwa kwa mamlaka zote za utekelezaji ukiwamo umoja wa
shule binafsi na taasisi inayosimamia shule za dini ya Kikristo na ile
ya shule za Kiislamu, hivyo hakuna kisingizio cha mtu kutopata huo
waraka… lazima wautekeleze,” alieleza Manori.
COMMENT AND SHARE..................!!!!!!!!
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!