Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe amesema amekuwa kimya muda mrefu kuhusiana na
kupotea katika mazingira ya kutatanisha, msaidizi wake Ben Saanane kwa
kuwa suala hilo lipo kwenye uchunguzi.
Mbowe alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
jijini Mbeya wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Kanda ya
Nyasa inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa.
Alisema yeye pia ameathiriwa na tukio hilo kama ilivyo kwa wazazi wake
na ndugu wengine kwa kuwa ni mtu muhimu kwake katika kutekeleza majukumu
yake.
“Ndugu zangu Watanzania msione nipo kimya, nimefanya hivi kutokana na
kuwa suala hili lipo kwenye uchunguzi kwani tukizidisha kuongea ongea
wale ambao wamemteka wanaweza kupoteza uhai wake kisa maneno,” alisema
Mbowe.
Alisema, “Chadema ni taasisi ambayo ina vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vinaendelea kuchunguza tukio hili la aina yake.”
Katika hatua nyingine, Mbowe aliishitumu Serikali akidai kwamba
imeendelea kuwafunga wanachama wake na kwamba mpaka sasa 180 wapo
mahabusu. Alisema hizo ni jitihada za kuua nguvu za upinzani.
Akijibu madai hayo, Kamishna wa Polisi (Operesheni na Mafunzo), Nsato
Marijani alisema jeshi hilo linawashikilia watu wengi kwa makosa
mbalimbali vituoni na wengine mahabusu katika magereza. Alisema polisi
haimkamati mfuasi wa chama cha siasa bali mtu anayekwenda kinyume cha
sheria.
“Hayo yanayosemwa siyo ya kweli, waache kulipaka tope jeshi la polisi.
Tutaendelea kuwakamata watu wote wanaovunja sheria. Hata kama akiwa
mjomba wangu tutamkamata.”
Msigwa kidedea
Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa
aliibuka kidedea baada ya kushinda kwa kupata kura za ndiyo 62 sawa na
asilimia 58.49 kati ya kura 106 zilizopigwa.
Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema (Bara), John Mnyika alisema nafasi ya makamu mwenyekiti
imechukuliwa na Sadrick Malila ambaye alipata kura za ndiyo 93 sawa na
asilimia 88 ya kura zilizopigwa 106 huku kura tatu zikiharibika.
Mnyika alisema kuwa nafasi ya mweka hazina imechukuliwa na Mbunge wa
Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda ambaye alishinda kwa
kupata kura 91 ambayo ni sawa na asilimia 86 kura zote 106 zilizopigwa.
Mnyika alisema katika uchaguzi huo wajumbe walipiga kura za ndiyo au
hapana kwa lengo la kufanya uchaguzi wa maridhiano kwani uchaguzi wa
kuweka wagombea wawili husababisha makundi na kuleta migogoro ndani ya
chama.
“Hivyo Kamati Kuu Taifa baada ya kuliona hilo tukaamua kuwaita wagombea
wote na kuwaeleza nia yetu ya kufanya hivyo na hatujafanya huku tu, hata
kanda nyingine tulizopita tumefanya hivyo"Alisema Mnyika
COMMENT AND SHARE.................................!!!!!!!!!!
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!