ZIFAHAMU NJIA ZA UZAZI WA MPANGO:;
Njia za uzazi wa mpango hutumika
na wanaume na wanawake kuzuia ujauzito kwa madhumuni ya kupanga uzazi ili kuwa
na familia bora. Ni vigumu kusema kuwa kuna njia iliyo bora zaidi ya uzazi wa
mpango kwa kuwa kila njia ina faida na hasara zake. Wote kati ya mwanamke na
mwanaume wana maamuzi juu ya mipangilio wa kupata watoto.
Kufanya uchaguzi utumie njia ipi
kwa ajili ya kupanga uzazi siyo kitu rahisi kwa kuwa kuna mambo mengi ya
kuzingatia kabla ya kufanya maamuzi yeyote. Lakini awali kabisa, inabidi
ujifunze njia mbali mbali, ili kuweza kubaini ni njia ipi itakayokufaa pamoja
na mwenzi wako kupanga uzazi. Mnaweza pia kuwasiliana na muuguzi au daktari
anayeusiana na masuala ya uzazi wa mpango kwa ushauri, ili muweze kuchagua njia
sahihi itakayowafaa.
Kabla ya kutumia njia yeyote ya
uzazi wa mpango, inabidi ufikirie kuhusu mambo yafuatayo:
- Afya yako kwa ujumla.
- Ni kwa kiwango gani njia husika ya uzazi wa
mpango inafanya kazi.
- Unajamiiana mara ngapi?
- Matarajio ya kupata mtoto siku za usoni.
- Je ni nini faida na madhara ya kutumia njia
husika ya uzazi wa mpango?
- Je unafurahia kutumia njia husika uliyochagua?
Yakupasa kufahamu kuwa, hata
kama njia unayotumia ni bora zaidi, wakati mwingine njia hiyo yaweza kushindwa
kufanya kazi. Lakini uwezekano wa kupata ujauzito utakuwa mdogo sana endapo
njia uliyochagua itatumika kwa usahihi wakati wa kujamiiana. Pia ikumbukwe pia,
njia za uzazi wa mpango za kutumia homoni na dawa, hazitakukinga na maambukizi
ya HIV na magonjwa ya zinaa.
Zifuatazo ni njia mbali mbali
ambazo zaweza kutumika kwa ajili ya uzazi wa mpango na jinsi zinavyofanya kazi.
Njia mojawapo ni njia ya asili ya kutumia kalenda.Kuifahamu zaidi njia hii
tembelea ukurasa wetu wa AFYA YA MAMA NA
MTOTO katika mtandao huu.
Njia nyingine ni ya dawa mseto za
vidonge vya kumeza. Vidonge hivi vina homoni za kutengeneza za estrogen na progestin. Dawa za vidonge vya uzazi wa mpango hufanya kazi kwa
kuzuia kutolewa kwa mayai kutoka katika ovari. Njia nyingine ya ufanyaji kazi
wa dawa hizi ni kuufanya ute ulio katika mlango wa uzazi kuwa mzito kiasi
kwamba huzuia mbegu za kiume kuogelea kulekea katika tumbo la uzazi na kuzuia
urutubishaji wa yai.
Huwa kuna aina tofauti za dawa za
vidonge vya uzazi wa mpango.Ni vyema ukawasiliana na daktari wako ili kuweza
kufahamu ni dawa gani itakayokufaa. Daktari wako anaweza kukushauri kutokutumia
dawa hizi kama:
- Una
tatizo la kuganda kwa damu katika mishipa ya damu.
- Umewahi kupata au una kansa ya matiti, kansa ya
ini au kansa ya kizazi.
- Kama ni mwanamama mwenye miaka zaidi ya 35 na
unavuta sigara.
- Kama unatumia aina fulani ya dawa za antibiotiki.
Dawa za antibiotiki zaweza kupunguza
uwezo wa ufanyaji kazi wa dawa za uzazi wa mpango, na mwanama anaweza kupata
ujauzito. Zungumza na mfamasia wako na daktari ili uweze kutumia njia mbadala
endapo utakua unatumia antibiotiki.
Plasta ya kubandika ni njia nyingine
ambayo hutumika kama dawa za uzazi wa mpango. Plasta hii hubandikwa katika
ngozi chini kidogo ya tumbo, kwenye mkono au paja na sehemu ya juu ya mwili kama kifuani. Plasta hii hutoa
homoni ya estrogen na progestrin na husharabiwa katika mfumo
wa damu. Dawa hii hufanya kazi kama ilivyo ya vidonge kwa kuzuia upevushaji wa
yai katika ovari. Pia huufanya ute wa mlango wa uzazi kuwa mzito na kuzuia
mbegu za kiume kupita kwenda kurutubisha yai. Kibandiko hiki cha plasta
hutumika mara moja wiki na kwa wiki tatu kila mwezi. Wiki ya nne mwanamama
hatotumia kibandiko hiki ili aweze kupata siku za hedhi kwenye mzunguko huo.
Dawa za kuchoma katika misuli na
husharabiwa kwenye mishipa ya damu kwa njia ya sindano kama Depo Provera®.
Mwanamama anayetumia njia hii huchomwa sindano ya homoni ya progestrin katika mkono kila baada ya miezi mitatu. Njia hii pia
huzuia upevushaji wa yai kutoka katika ovari na kuufanya ute wa njia ya uzazi
kuwa mzito na kuzuia mbegu za kiume. Dawa hii isitumike zaidi ya miaka miwili
kwa kuwa yaweza kusababisha tatizo la mifupa ambalo huisha baada ya kuacha.
Endapo itatumika kwa muda mrefu zaidi ya hapo yaweza kusababisha udhaifu wa
mifupa (kitaalam kama osteoporosis).
Ringi ya kuweka kwenye uke ni njia nyingine ambayo hutoa
homoni za estrogen na progestrin. Na hii vile vile hufanya
kazi kwa kuzuia upevushaji wa yai katika ovari na huufanya ute wa njia ya
mlango wa uzazi kuwa mzito na kuzuia mbegu za kiume kupita. Mwanama huibinya
ringi katikati kwa kutumia
kidole gumba na cha shahada na
kuingiza ndani ya uke. Ringi hii huvaliwa kwa wiki tatu na hutolewa mwanamama
anapoona siku zake za hedhi na hutumia ringi mpya katika mzunguko unaofuata.
Kipandikizi(kijiti) ni aina ya kifaa
chenye ukubwa wa kadiri ya njiti ya kiberiti, hujikunja kwa urahisi na huwekwa
chini ya ngozi kwenye sehemu ya juu ya mkono. Kipandikizi hutoa homoni ya progestrin ambayo hubadilisha hali ya
ukuta wa uzazi na pia kuufanya ute wa njia ya uzazi kuwa mzito na kuzuia yai
kurutubishwa.Njia hii huweza kufanya kazi kwa muda wa miaka mitatu.Muuguzi au
daktari atamsaidia mwanamama kuweka kipandikizi.
Kipandikizi cha kwenye tumbo la
uzazi(intrauterine devices-IUD),
chenye umbo la herufi “T”, Kifaa hiki kidogo huwekwa katika tumbo la uzazi na
kuna aina mbili za kifaa hiki:
- Kipandikizi cha shaba(Copper IUD),kifaa hiki hufanya kazi kwa kutoa kiasi kidogo cha
madini ya shaba katika tumbo la uzazi na kuzuia mbegu za kiume kurutubisha yai,
kama yai litarutubishwa madini haya yatazuia yai hilo lisipandikizwe katika
ukuta wa uzazi. Mwanamama atahitaji usaidizi wa daktari katika uwekaji wa kifaa
hiki. Kifaa hiki chaweza kubaki kikiendelea kufanya kazi kwa muda wa miaka
mitano hadi kumi.
- Kipandikizi chenye homoni (Hormonal IUD) kifaa hiki ambacho hupatika kwa jina la Mirena®,
hutoa homoni ya progestrin katika
tumbo la uzazi na kuzuia upevushaji wa yai pamoja na kuufanya ute wa njia ya
kizazi kuwa mzito na kuzuia urutubishaji. Huzuia pia yai lililorutubishwa
kupandikizwa katika ukuta wa uzazi.
Usaidizi wa daktari huitajika katika uwekaji wa kifaa hiki ambacho hudumu hadi
kufikia miaka mitano.
Baada ya kujifungua mwanamama
apate ushauri wa daktari kabla ya kutumia dawa za uzazi wa mpango zenye homoni
za estrogen na progestrin. Dawa hizi zaweza kuongeza hatari ya kuganda kwa damu,
tatizo ambalo hujitokeza baada ya kujifungua. Wakinamama waliojifungua kwa njia
ya upasuaji au wana matatizo yanayoweza kusababisha kuganda kwa damu, uzito
mkubwa, historia ya damu kuganda, wanavuta sigara, au kifafa cha mimba
wanahitajika kusubiri angalau kwa wiki sita, hii ni baada ya kujifungua.
Kufunga uzazi kwa njia ya
kipandikizi (sterilization implant),hii
ni njia ya kufunga uzazi bila upasuaji kwa kinamama. Huu ni mrija mwemba ambao
hutumika kuingiza koili ndogo kwenye kizazi hadi kufikia mirija ya kupitisha
mayai (fallopian tubes).Kifaa hiki
hufanya kazi kwa kusabisha tishu za kovu kutengenezwa katika mirija ya uzazi na
kuziba njia ya kupitisha mayai. Kutengenezwa kwa kovu huchukua muda wa miezi
mitatu, kwa hiyo katika kipindi hicho, mwanamama hushauriwa kutumia njia
nyingine za uzazi wa mpango. Baada ya miezi mitatu mwanamama hutakiwa kwenda
hospitali kuchunguzwa kama kovu lilijitengeneza na kuziba kabisa mirija ya
kupitisha mayai.
Kufunga uzazi kwa njia ya
upasuaji (surgical sterilization), kwa njia hii upasuaji hufanyika na kufunga
mirija ya kupitishia mayai aidha kwa kuikata mirija, kuifunga au kuiziba.Hii
huzuia mayai kupitishwa kwenda kwenye tumbo la uzazi. Upasuaji huu pia waweza
kufanywa mwanamama anapojifungua kwa njia ya upasuaji ili kuepusha upasuaji
mwingine.
Njia hii kwa wanaume hujulikana
kama
vasectomy, ambapo kwa kuikata au
kuifunga mirija ya kupitisha mbegu za kiume hufanya mwanaume kutoa maji maji
yasiyo na mbegu hizi na hivyo kutokuwa na uwezo wa kumpa mimba mwanamke. Mbegu
za kiume zaweza kubaki katika mfumo wa uzazi wa mwanaume kwa miezi mitatu baada
ya upasuaji, kwa hiyo njia nyingine za uzazi wa mpango hazina budi kutumika ili
kujikinga na ujauzito usiotarajiwa. Baada ya muda huo utafiti mdogo hufanyika
kuhakiki uwepo wa mbegu hizo.

Katika sehemu ya kwanza tuliona
uchaguzi kufahamu utumie njia ipi kwa ajili ya kupanga uzazi.Uchaguzi wa njia hizi siyo kitu rahisi
kwa kuwa kuna mambo mengi ya kuzingatia kabla ya kufanya maamuzi yeyote. Lakini
awali kabisa, inabidi ujifunze njia mbali mbali, ili kuweza kubaini ni njia ipi
itakayokufaa pamoja na mwenzi wako kupanga uzazi. Mnaweza pia kuwasiliana na
muuguzi au daktari anayeusiana na masuala ya uzazi wa mpango kwa ushauri, ili
muweze kuchagua njia sahihi itakayowafaa.Pia tulijifunza kuhusu njia mbali
mbali tukiangalia faida na hasara zake.Zifuatazo ni njia nyinginezo
ambazo zaweza pia kutumika kupanga uzazi. Njia hizi ni kama njia ya dharura na njia za
vizuizi.
Njia ya dharura za uzazi wa
mpango huusisha matumizi ya dawa za kumeza(morning
after pills). Njia hii humsaidia mwanamama asipate ujauzito endapo atajamiiana
bila kutumia njia yeyote, au pengine njia aliyoitumia kwa ajili ya kupanga
uzazi haikutumika kwa usahihi au haikufanya kazi (mfano kupasuka kwa mpira wa kiume). Kuna wakati pia mwanamama anaweza
kusahau kumeza vidonge vya uzazi wa mpango.
Njia hii ya dharura imekuwa
muhimu sana kwa watoto wa kike na kinamama wanaotendewa ukatili kwa kubakwa au
kushawishiwa kushiriki katika vitendo vya ngono na watu wenye hila mbaya.
Dawa za dharura za uzazi wa
mpango hutumiwa katika dozi moja au dozi mbili. Dawa iliyo na dozi moja hufanya
kazi sawa na ile iliyo na dozi mbili. Dawa hii ya homoni hufanya kazi kwa kuzuia
upevushaji wa yai katika ovari au kuzuia mbegu za kiume (sperm) kurutubisha yai. Dawa hii hutumika kabla ya saa 72 kupita
baada ya mwanamama kujamiaana bila kutumia njia yeyote kupanga uzazi.
Vizuizi ni aina nyingine za njia za
uzazi wa mpango ambazo haziusishi matumizi ya dawa za homoni .Njia mojawapo hujulikana kama kiwambo (diaphragm). Kiwambo hiki hutengenezwa kwa kutumia mpira na chenye umbo la bakuli ndogo.
Kiwambo hiki hupatikana katika ukubwa tofauti, na mwanamama atahitaji msaada wa
daktari ili aweze kufahamu ukubwa wa kiwambo kitakachomfaa. Uwekaji wake
hautahitaji msaada wa daktari kama ilivyo kwa vipandikizi.
Kabla ya kujamiaana mwanamama
hukiweka kiwambo kufunika mlango wa kizazi (cervix).
Kiwambo hufanya kazi kwa kuzuia mbegu za kiume kuogelea kuelekea tumbo la uzazi
na huitaji kuondolewa ndani ya muda wa saa 24.
Mipira ya kike(female condom), ni aina nyingine ya
kizuizi, ambayo huvaliwa na mwanamama katika uke. Njia hii hufanya kazi kwa
kuzuia mbegu za kiume kuingia katika tumbo la uzazi.Aina hii ambayo
hutengenezwa kwa mpira mwembamba ina ringi mbili.Ringi ya ndani(iliyo ndogo)
ambayo huingizwa na kujishika kwa ndani na ringi ya nje(iliyo kubwa) huzuia
sehemu ya nje ya mpira kuingia ndani ya uke wakati wa kujamiiana. Mpira huu
waweza kuvaliwa masaa 8 kabla ya kujamiina na humpa uhuru zaidi mwanamama
katika maamuzi ya kutumia mpira ukilinganisha na mipira ya kiume. Mpira
utahitajika kubadilishwa endapo mwanamama atajamiiana tena. Mpira huu usitumike
pamoja na mpira wa kiume kwa wakati mmoja.
Mpira wa kiume(male condom),
huvaliwa kwenye uume baada ya kuhemka.Aina hii ya kizuizi hutengenezwa kwa
mpira (latex,polyurethane).Kila
wakati mwanaume anapojamiaana huitaji kubadilisha mpira mpya.
Ili isipoteze ubora wake mipira
ya kiume na kike inahitaji kuhifadhiwa sehemu kavu na isiyo na joto. Epuka
kutumia vilainishi vya mafuta kwa kuwa huaribu mpira na waweza kupasuka.Vilainishi
kama gel zinazochanganyika na maji zaweza kutumika mfano K-Y Gel®.
Je njia zote za uzazi wa mpango zaweza kuzuia HIV na magonjwa ya zinaa?
Jibu ni hapana. Mpira wa kiume
ndiyo njia pekee iliyofanyiwa utafiti na kuonekana kuwa na uwezo wa kukinga
magonjwa ya zinaa na HIV ingawa siyo kwa asilimia mia moja. Tafiti zinaendelea
kuchunguza mipira ya kike kama yaweza kuzuia maambukizi ya HIV na magonjwa
ya zinaa.
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!