Vikwazo vitano katika safari ya Ujasiriamali na njia Tano za kuvikabili:;
Tunaishi kwenye zama ambazo ni muhimu sana kwa mtu kuwa mjasiriamali.
Hii ni kwa sababu kumekuwa na mabadiliko makubwa sana kiuchumi ambayo
yametoa nafasi kwa watu kuweza kuingia kwenye ujasiriamali na
kufanikiwa. Ukosefu wa ajira na pia changamoto wanazopata watu kwenye
ajira zinawasukuma watu kuingia kwenye ujasiriamali. Pia maendeleo ya
kiteknolojia yamerahisisha sana ujasiriamali. Kukua kwa mtandao wa
intaneti na uwepo wa mitandao ya kijamii umefanya mtu kuweza kuuza
bidhaa au huduma zake katika mataifa ya mbali bila ya yeye kusafiri au
kutumia gharama kubwa.
Pamoja na mazingira haya mazuri yanayowavutia watu kuingia kwenye
ujasiriamali bado sio wote wanaoingia kwenye ujasiriamali wanapata
mafanikio makubwa na hata kukua. Ukweli ni kwamba watu wengi wanaoingia
kwenye ujasiriamali au wanaoanza biashara, biahsara zao zinaishia kufa
ndani ya muda mfupi. Hata wale ambao biashara zao hazifi, zinaishia
kudumaa na kushindwa kukua zaidi. Kuna watu wengi ambao wamekuwa
wanafanya biashara ya aina moja miaka mingi bila ya kuona mabadiliko
makubwa kwao na kwa biashara wanayofanya.
Leo, hapa
tutajadili vikwazo mbalimbali vilivyopo kwenye safari ya ujasiriamali
na jinsi ambavyo unaweza kuvivuka ili uweze kufikia mafanikio makubwa
kupitia ujasiriamali wako.
Vifuatavyo ni vikwazo vilivyopo kwenye safari ya ujasiriamali
vinavyowazuia wajasiriamali wengi kushindwa kufikia mafanikio makubwa.
i) Mtazamo wa mjasiriamali mwenyewe
Watu wengi wanapofikiria kuingia kwenye biashara au ujasiriamali
huamini kwamba wanakuwa mabosi wao wenyewe na hivyo hakuna wa
kuwapelekesha. Hakuna mtu anayeweza kuwafanya waamke asubuhi na mapema
kutekeleza majukumu yao, wafanye kazi muda wa ziada au hata kufanya vitu
wasivyopenda kufanya. Kwa mtazamo huu mjasiriamali anayeanza anakuwa
anafanya mambo kwa muda anaojisikia mwenyewe na hivyo kushindwa kuwa na
uzalishaji mkubwa. Unapoingia kwenye ujasiriamali, hasa wakati wa
mwanzoni unahitaji kufanya kazi zaidi hata ya mtu ambaye ameajiriwa. Mtu
aliyeajiriwa anafanya kazi masaa nane mpaka kumi kwa siku na siku tano
kwa wiki. Mjasiriamali anaweza kujikuta anafanya kazi masaa zaidi ya
kumi na mbili kwa siku na wakati mwingine siku saba kwa wiki. Kufikiri
kwamba kuwa kwenye ujasiriamali au biashara ni kufanya kile
unachojisikia kufanya kwa wakati unaomamua mwenyewe ni kikwazo kikubwa
cha watu wengi kufanikiwa kwenye ujasiriamali.
ii) Ushindani mkali
Changamoto nyingine wanayoipata wajasiriamali ni ushindani mkali ambao
wanakutana nao wanapoingia kwenye biashara. Mara nyingi watu wanapoingia
kwenye biashara kwa mara ya kwanza huangalia ni biashara gani inalipa
na wao kujiingiza kwenye biashara kama hiyo. Unapokuwa nje na kabla ya
kuingiakwenye biashara unaweza kuona inalipa vizuri sana. Unaweza kuweka
mipango mikubwa na mizuri sana na kuona ukiingia ni jinsi gani unaweza
kupata faida kubwa. Ila unapoingia kwenye biashara husika ndipo
unapokutana na ukweli ambao hukuweza kuuona mwanzoni wakati unapanga.
Unapoingia kwenye biashara unaona jinsi ambavyo ushindani ni mkubwa na
wale ambao wamekutangulia wanakuwa na uwezo mkubwa wa kuhimili ushindani
huo kuliko wewe unayeanza. Hii imekuwa ikiwafanya wengi wanaoingia
kwenye biashara kushindwa na hatimaye kluacha kabisa biashara hiyo.
iii) Mtazamo wa wanaokuzunguka
Kuwa mjasiriamali au mfanyabiashara kwenye mazingira ya nchi masikini
kama Tanzania, kila mtu anaangalia jinsi ya kukurudisha nyuma. Hii ni
kwa sababu kila mtu anapenda kupata zaidi kwa gharama kidogo. Hivyo
unaweza kuanza biashara kwa kushirikiana na mtu au watu wengine na wao
wakataka kufaidi kuliko unavyofaidi wewe. Unaweza kuajiri wa fanyakazi
na wao wakawa ndio watu wa kwanza kukuibia. Na hata ndugu zako wa karibu
wanapoona unafanya biashara wanaweza kuamini kwamba wewe unapata faida
kubwa na hivyo kutegemea wewe uwasaidie. Mambo haya ni changamoto kubwa
sana hasa mwanzoni mwa biashara ambapo unahitaji kukua zaidi ya kuondoa
fedha kwenye biashara.
iv) Kufanya vitu kwa mazoea na kutokupenda kujifunza
Ujasiriamali unahitaji kujifunza kila siku na kuwa mbunifu kila mara.
Watu wengi hawapendi kusumbua vichwa vyao kufikiri zaidi. Wanapenda
kufanya kile ambacho wamezoea kufanya, wanapenda kufanya walichofanya
jana. Hii inawafanya kuingia kwenye changamoto kubwa sana ya kushindwa
kubadilika kadiri mazingira yanavyobadilika. Kwa kushindwa kubadilika
wanazidi kubaki nyuma na kujiweka katika nafasi ya kuweza kushindwa pale
unapotokea ushindani.
Kujifunza kila siku ni hitaji muhimu sana ili kuweza kufanikiwa kwenye
biashara na ujasiriamali. Dunia ya sasa mambo yanabadilika kwa kasi
kubwa sana. Kuna taarifa muhimu sana unazotakiwa kuzipata kuhusiana na
biashara unayofanya na hata biashara kwa ujumla. Utazipata taarifa hizi
kama unapenda kujifunza na hata kusoma mambo yanayoendana na biashara.
v) Matatizo ya kifedha
Fedha ndio damu ya biashara yoyote ile, kama ilivyo damu kwenye mwili
wa binadamu. Mzunguko mzuri wa fedha kwenye biashara ndio utaifanya
biashara iwe hai na iendelee kukua. Matatizo yoyote kwenye mzunguko wa
fedha yanaweza kupelekea kufa kwa biashara kama ambavyo mtu atakufa kama
akipatwa na matatizo makubwa kwenye mfumo wake wa damu.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanashindwa kutofautisha matumizi yao
binafsi na matumizi ya biashara zao. Hivyo wamekuwa wakitumia fedha
inayotoka kwenye biashara moja kwa moja na hivyo kutumia kile
wanachozalisha. Hii inawafanya kushindwa kujua kama wanatengeneza faida
au wanapata hasara na mwishowe wanashindwa kujua kama wanakua, wamedumaa
au wanarudi nyuma.
Changamoto hizi zimekuwa kikwazo kikubwa kwenye maendeleo ya
ujasiriamali na biashara. Na kama tulivyoona kwenye changamoto hizo,
nyingi zinaweza kuzuilika au kuondolewa kabisa na mfanyabiashara akaweza
kuona faida kutokana na biashara anayofanya.
Msomaji
,
yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo mfanyabiashara anaweza kufanya ili
kuepuka changamoto zinazoweza kumwondoa kwenye biashara.
1. Jua kwamba biashara au ujasiriamali ndio kazi yako na inakuhitaji sana ili kukua
Kama upo kwenye ujasiriamali au unapanga kuingia kwenye ujasiriamali ni
muhimu kujua kabisa ya kwamba safari hii ya ujasiriamali sio rahisi. Ni
safari ambayo inahitaji wewe kujitoa, uwe tayari kufanya kazi kwa muda
mrefu zaidi ya watu walioajiriwa na uwe tayari kufanya kazi nyingi zaidi
ya mtu aliye kwenye ajira. Unapoanzisha biashara yakounaweza kuvaa
kofia nyingi sana kwa wakati mmoja, unaweza kuwa wewe ndio mmiliki wa
biashara, wewe ndio afisa masoko, wewe ndio mhasibu, wewe ndio mtafiti
na wewe ndio afisa mauzo. Ni lazima uyajue maeneo yote muhimu ya
biashara yako ili kujua ni wapi panahitaji nguvu zaidi ili uweze kukua
zaidi. Ni lazima uweze kujidukuma kufanya kazi hata pale ambapo
hujisikii kufanya hivyo. Na jambo muhimu sana kwenye safari ya
ujasiriamali ni kwamba unahitaji kuweza kujiongoza mwenyewe. Usiwe ni
mtu ambaye unasubiri kupangiwa nini cha kufanya au kusukumwa ndio uweze
kutekeleza majukumu yako.
2. Kuwa mbunifu na jitofautishe na wengine
Unaweza kuingia kwenye biashara kwa kuangalia ni biashara gani
inayotoka kwa maeneo unayotaka kufanyia biashara ila usitegemee biashara
yako kukua kwa kufanya kile ambacho kila mtu anafanya. Unahitaji kuwa
na ubunifu mkubwa na kuweza kujitofautisha na wafanyabiashara wengine
wanaofanya biashara kama unayofanya wewe. Fikiria jinsi ambavyo unaweza
kufanya biashara yako tofauti na ukawavutia wateja wengi zaidi. Angalia
ni vitu gani ambavyo ni muhimu kwa ukuaji wa biashara hiyo na ambavyo
wafanya biashara wengine hawavifanyi kisha vifanye. Hii itakufanya wewe
kuwa wa pekee na hivyo kuondoka kwenye ushindani ambao utakuumiza
kichwa. Katika kila biashara kuna jambo linaloweza kuboreshwa zaidi na
kuifanya biashara kukua zaidi.
3. Shirikiana na watu ambao unaweza kuwaamini na wanapenda kufanya biashara unayofanya
Kama unahitaji kushirikiana na mtu ili kuanzisha biashara hakikisha
unashirikiana na mtu ambaye unamjua vizuri na unaweza kumuamini. Mtu
huyo awe na rekodi nzuri ya kufanya mambo kwa uaminifu ili muweze
kuaminiana kwenye biashara. Na pale unapoajiri ajiri watu wenye uwezo,
waaminifu na ambao wanapenda kufanya biashara hiyo ambayo unawaajiri.
Kuajiri mtu ambaye anataka tu kupata mshahara atakuwa mzigo kwako hasa
kwenye kipindi ambapo biashara inakuwa ngumu.
4. Kuwa na usimamizi mzuri wa fedha kwenye biashara yako
Cha kwanza kabisa kwenye usimamizi wa fedha za biashara yako,
itofautishe biashara yako na wewe binafsi. Matumizi ya biashara yafanye
tofauti kabisa na matumizi yako binafsi. Jua mauzo ya biashara yako na
faida unayoipata baada ya kuondoa matumizi yote ya biashara. Pia
matumizi yako yaweke kwenye biashara kama mshahara ambao unajilipa. Hii
itakufanya uweze kuona kama biashara yako inakua au inadidimia.
5. Kuwa mvumilivu
Hakuna kitu chochote unachoweza kufanikiwa kwenye maisha kama hutakuwa
na uvumilivu. Utakutana na vikwazo vingi sana kwenye safari yako ya
biashara. Kuna wakati ambapo utaona unashindwa kabisa ila unapokata tama
ndio unakubali kujiondoa kwenye njia ya mafanikio. Kuwa mvumilivu na
jifunze kupitia changamoto unazopata, kama kuna kitu umekosea na
kikakugharimu jifunze kupitia kitu hiko na usikirudie tena. Jinsi
unavyokutana na changamoto nyingi ndio unazidi kujifunza na kukomaa.
Mafanikio kwenye ujasiriamali na biashara sio kitu ambacho kinatokea
mara moja na kwa haraka. Ni kitu ambacho kinahitaji muda, kufanya kazi
kwa bidii na maarifa na kuwa mvumilivu. Wafanyabiashara wakubwa
tunaowaona leo hawakuanzia walipo sasa, walianzia chini kabisa na juhudi
na uvumilivu ndio vimewafikisha walipo.
Msomaji
,
amua na wewe kuwa mmoja wa wafanyabiashara watakaokuwa wakubwa sana ili
kujiletea maendeleo wewe binafsi, wale wanaokuzunguka na hata taifa kwa
ujumla. Hakuna kinachoshindikana kama kweli utajitoa. Nakutakia kila la
kheri katika mafanikio kupitia ujasiriamali mwaka 2016!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!