UTI, UGONJWA UNAOATHIRI MFUMO WA NJIA YA MKOJO:;
UTI(Urinary tract infections) ni uambukizi wa njia ya mkojo ambao
huwasumbua watu wengi siku hizi. Uambukizi huu unaweza kusababisha maumivu na
kukosa raha, na ugonjwa waweza kudumu kwa siku chache kama utawahi kutibiwa kwa
kutumia dawa za antibiotiki.Kuna uwezekano pia wa kuchukua hatua kuhakikisha
unaepukana na maambukizi haya ya njia ya mkojo.
UTI ni ugonjwa ambao huwaathiri zaidi wanawake ukilinganisha na
wanaume, na sababu kubwa ikiwa ni ya kimaumbile, ingawa kuna sababu nyingine
kama kufanya ngono na historia ya kifamilia.
Watoto pia waweza kuathirika na ugonjwa huu wa UTI, husani watoto wa
kike walio chini ya umri wa miaka miwili na watoto wa kiume wasiotahiriwa.
Dalili kuu kwa watoto wenye ugonjwa huu ni homa, ingawa vipimo huhitajika ili
kuhakikisha uwepo wa ugonjwa. Wazee nao pia huweza kuathirika na
ugonjwa huu.
Mfumo wa mkojo ni ule ambao miili yetu hutengeneza na hata kuutoa
mkojo nje ya mwili. Na unahusisha sehemu kuu nne:-
- Figo(Kidney),
ambazo ni ogani zilizo na umbo la haragwe na zinakuwa mbili, na ukubwa wake ni
kadirio la unavyokunja ngumi yako. Kazi ya figo ni kuchuja damu na matokeo yake
ni mkojo unaotengenezwa na hutolewa kama uchafu
mwilini.
- Mirija ya kutoka figo kwenda kwenye kibofu( ureters), huwa ni miwili na hupeleka
mkojo kwenda kwenye kibofu.
- Kibofu, ambacho kazi yake ni kukusanya na
kuhifadhi mkojo unaotoka katika figo,mkojo hutolewa pale mtu anapoamua kukojoa.
- Mrija wa kutoa mkojo kutoka kwenye kibofu(urethra), huu ni mrija mmoja ambao hutoa
mkojo nje mtu anapoamua kukojoa.
UTI husababishwa kwa kiasi kikubwa na bakteria ambao huingia katika mrija
wa kutoa mkojo kutoka katika kibofu. Asilimia kubwa ya ugonjwa huu katika jamii
husababishwa na bakteria ajulikanaye kama Escherichia
coli(E Coli), Pia asilimia ndogo yaweza kusababishwa na aina nyingine ya
bakteria ajulikanaye kama Staphylococcus
saprophyticus.Lakini pia kwa uchache sana ugonjwa waweza kusababishwa na
fangasi au virusi.
Ugonjwa huu ambao hauko katika kundi la magonjwa ya zinaa, lakini
kufanya ngono wakati mwingine husababisha kuambukizwa kwa ugonjwa huu
Dalili za UTI hutofautiana kulingana na sehemu ya njia ya mkojo
iliyoathirika.
Jedwali
Sehemu iliyoathirika
|
Dalili
|
Figo
|
- Kichefuchefu.
- Kutapika.
- Maumivu ya mgongo wa juu.
- Homa kali.
- Kutetemeka na kusikia baridi
|
Kibofu
|
- Damu katika mkojo.
- Maumivu ya nyonga.
- Maumivu chini ya kitovu.
- Kukojoa mara kwa mara na kupata maumivu wakati
wa kukojoa.
|
Mrija wa kutoa mkojo kutoka kwenye kibofu (urethra)
|
- Mkojo wa kuunguza wakati wa kukojoa(maumivu
njia ya mkojo)
|
Siyo mara zote ambazo mtu hupata dalili za ungonjwa huu, lakini
zinapotokea huwa ni kama ifuatavyo:- Kujisikia haja ya kukojoa mara kwa mara,
kusikia maumivu wakati wa kukojoa, kukojoa mara kwa mara mkojo kidogo, mkojo wa
rangi ya mawingu mawingu, mkojo mwekundu au pink, pia wa rangi ya brauni, mkojo
unaotoa harufu, maumivu ya nyonga kwa wanawake na maumivu kwenye njia ya haja
kubwa kwa wanaume. Endapo utakuwa na dalili hizo zilizotajwa awali ni vyema
kupata ushauri wa daktari.
Uambukizi wa njia ya mkojo hutokea kama bakteria wataingia katika
mrija wa kutoa mkojo kutoka katika kibofu, na huzaliana na kuongezeka katika
kibofu. Ingawa bakteria hawa waweza kuishi katika kibofu bila kuleta madhara,
lakini wakati mwingine kinga ya mwili hushindwa kufanya kazi ipasavyo na uambukizi
hutokea. Uambukizi unapotokea ndipo mgonjwa anaweza kuona dalili mbalimbali
tulizoziona awali.
Kama tulivyoona awali mara nyingi ugonjwa huu huwaathiri zaidi
wanawake na sababu kubwa ikiwa ni ya maumbile.
- Uambukizi katika mrija wa kutoa mkojo kutoka
katika kibofu (Infection of the urethra)-Aina
hii ya UTI hutokea endapo bakteria wanaopatikana tumboni watasambaa kutoka njia
ya haja kubwa na kuingia katika mrija wa mkojo. Na kwa kuwa mrija wa kutoa
mkojo uko karibu uke mwanamke anaweza pia kuambukizwa UTI kwa kufanya ngono,
ambapo vijimelea kama gonococcus na chlamydia vinaweza kusabisha aina hii
ya UTI.
- Uambukizi katika kibofu- Aina hii ya UTI mara
nyingi husababishwa na bakteria aina ya E coli, bakteria hawa hupatikana tumboni.Maumbile ya uke kuwa karibu ya njia ya
aja kubwa huchangia sana bakteria hawa kuweza kuingia kwa urahisi katika njia
ya mkojo na kusababisha uambukizi.
Walio katika hatari ya kupata
ugonjwa.
- Wagonjwa walioingiziwa mpira wa kusaidia kutoa
mkojo(catheter) huwa katika hatari
kubwa ya kupata UTI. Hii inajumuisha wagonjwa waliolazwa, wenye matatizo ya magonjwa
ya fahamu na hawawezi kutoa mkojo, pia wagonjwa waliopooza.
- Wagonjwa walio na kinga ya mwili iliyoshuka,
mfano wale wenye kisukari na magonjwa mengineo yanayoshusha kinga ya mwili
dhidi ya vijimelea vya magonjwa, wanakuwa katika hatari ya kupata ugonjwa huu.
- Wagonjwa walioziba njia ya mkojo, hii inaweza
kusababishwa na mawe ya kwenye figo na kukua kwa tezi dume kwa wanaume, hii
husabisha mkojo wenye bakteria kushindwa kutoka na kusababisha uambukizi katika
kibofu na figo.
- Hitilafu katika njia ya mkojo- inawezekana mtoto
kuzaliwa na hitilafu hii ambayo husababisha mkojo kushindwa kutoka kwa urahisi
na kuchochea maambukizi haya ya UTI.
- Ukomo wa hedhi, hii ni kwa sababu homoni ya
ostrogeni hupungua na kusababisha mabadiliko katika njia ya mkojo.
- Matumizi ya njia za uzazi wa mpango, ambayo vipandikizi
huwekwa katika njia ya kizazi(diaphragm).Yaweza
pia kuchochea kupata maambukizi haya.
- Kuwa katika umri wa matamanio ya kufanya ngono.
Wanawake walio katika umri wa matamanio ya ngono wameonekana kuthirika zaidi ya
wale wasio na matamanio ya ngono.
- Kuwa mwanamke, wanawake wana mrija mfupi wa
kutoa mkojo kutoka katika kibofu ukilinganisha na wanaume. Kwa hiyo huwa ni
rahisi kwa bakteria kufikia kibofu kwa wanawake, na kupata uambukizi.
Ugonjwa wa UTI unapotibiwa mapema, hupona kwa urahisi na hakuna
madhara yeyote atapata mgonjwa. Lakini ugonjwa usipotibiwa na kuwa sugu madhara
huweza kutokea. Madhara haya ni kama kuharibika kabisa kwa figo endapo mgonjwa
ataishi na ugonjwa kwa muda mrefu bila kutibiwa. Athari hizi huwa ni zaidi kwa
watoto ukilinganisha na watu wazima. Mwanamama mjamzito asiyetibiwa ugonjwa,
anaweza kujifungua mtoto mwenye uzito mdogo au aliye njiti.
Mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa hufanyiwa vipimo vya kimaabara. Kwa
uchunguzi zaidi bakteria huoteshwa katika maabara ili kuweza kugundua ni aina
gani ya bakteria waliosababisha ugonjwa na uchunguzi huu husaidia katika kuchagua tiba
iliyo sahihi.
Vipimo vingine vya picha za ndani ya mwili vyaweza kutumika ili
kuchunguza endapo mgonjwa amepata madhara katika njia ya mkojo. Vipimo hivi ni
kama CT scan, ultrasound na X ray .
Pia mkojo waweza kuchunguzwa katika maabara kuangalia uwepo wa
chembechembe za seli nyeupe za damu, seli nyekundu za damu au hata uwepo wa
bakteria. Ni vyema mgonjwa anapotoa mkojo wa uchunguzi kuhakikisha mkojo huo
hauingii vijimelea kutoka katika mazingira ya anapotolea mkojo huo.
Kamwe usitumie dawa bila ya kupata ushauri wa daktari na vipimo
kuhakikisha aina ya ugonjwa. Baada ya vipimo onana na mfamasia kwa ajili ya
dawa na ushauri kuhusu matumizi ya dawa.
Kwa ugonjwa usio sugu dawa kama Sulfamethoxazole-trimethoprim (Septrin)
yaweza kutumika, Amoxiccilin+clavulanic acid (Augumentin), Nitrofurantoin na
Ciprofloxacin zaweza kutumika kutibu ugonjwa.
Kwa kawaida dalili za ugonjwa hutoweka siku chache baada ya kuanza
kutumia dawa, lakini hiyo siyo sababu ya kuacha kutumia dawa. Unaweza hitajika
kutumia dawa zako kwa muda wa zaidi ya siku saba ili upone kabisa. Tumia kozi
nzima ya antibiotiki kama ulivyoelekezwa na mfamasia wako ili kuhakikisha uambukizi
unamalizika kabisa. Pia waweza kupewa dawa za kuondoa maumivu katika njia ya
mkojo.
Mgonjwa anaweza kutibiwa pia kwa kuongezewa ostrogeni kama UTI
inaambatana na ukomo wa hedhi (postmenopausal
UTI)
Uambukizi ulio sugu hutibiwa baada ya uoteshaji wa bakteria katika
maabara ili kuweza kugundua antibiotiki ifaayo zaidi. Mara nyingi mgonjwa huwa
na kozi ndefu ya antibiotiki, na mara nyingine huitajika antibiotiki za kutumia
kwa njia ya mishipa ya damu (Sindano)
Jinsi ya kujikinga na UTI
- Epuka bidhaa za wanawake zenye antiseptiki,
bidhaa hizi huuwa bakteria wenye faida(normal
flora) na wanaoimarisha kinga ya mwili kwenye uke. Bidhaa hizi kama
dochi,poda, sabuni, deodoranti zaweza kusababisha upate uambukizi kwa urahisi.
- Jifute kuanzia mbele kwenda nyuma, hii ni baada
ya haja ili kuepuka kuwapeleka bakteria wa tumboni katika mrija wa mkojo.
- Kunywa vimiminika kwa wingi, hususani maji,hii
husaidia kupata mkojo mwingi na kukojoa mara nyingi na kuwaondoa bakteria
kutoka katika kibofu na kuepuka uambukizi.
- Hakikisha bafu na choo vinafanyiwa usafi wa hali
ya juu.
- Hakikisha vyombo na vifaa vya bafuni na chooni
ni visafi na maji yanayotumika pia ni safi. Waweza kutumia water guard kuhakikisha maji ya bafuni na chooni ni safi.
- Matumizi ya tamponi yahitaji usafi wa hali ya
juu, kwa kuwa waweza kuingiza katika uke bakteria wasababishao ugonjwa.
- Wanawake
waepuke nguo zinazobana, Nguo zisizobana husababisha uke kupata hewa na
kuwa mkavu na kuepuka uvamizi wa bakteria. Epuka
suruali za jeans zinazobana hususani
katika maeneo yenye joto. Chagua nguo za ndani zenye fiba za asili, mfano nguo
za pamba.
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!