Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia
ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, mwili wako
unahitaji virutubishi ili kusaidia ukuaji wa mwili, kama ni kijana mwili
wako una mahitaji maalumu unayoyahitajia kudhamini makuzi ya kiafya ya
mwili wako wakati wa utu uzima na wakati unapokuwa mtu mzima unahitaji
kuwa na uzito uliolingana na mwili wa wastani.
Tukiangalia katika
upande wa Akina mama wajawazito na wale wanaonyonyesha nao pia wana
vyakula vyao maalumu wanavyohitajia tofauti kabisa na wanawake wengine.
Uchunguzi wa kitiba uliofanywa unaonyesha kuwa, hali ya kiafya ya mama
mjazito huwa na athari mbalimbali kwa mtoto atakayezaliwa. Vile vile
kuna ushahidi mkubwa kuwa magonjwa sugu ya watu wazima huanzia wakati
mtoto bado akiwa tumboni mwa mama yake akiwa katika hali ya kiluilui au
(foetus). Kwa hivyo akina mama wajawazito wanashauriwa kuzingatia
vyakula wanavyokula kabla na baada ya kushika mimba. Sasa tuangalie
athari za chakula kwa afya ya mtoto na virutubisho vinavyopaswa
kujumuishwa katika mlo wa mama mjamzito. Chakula cha mama mjamzito
kinaweza kuwa na athari kubwa muhimu kwa afya ya watoto kwa miaka mingi
baada ya kuzaliwa. Miaka kadhaa ya hivi karibuni, Jarida la Masuala ya
Lishe la Uingereza la Prestigious lilichapisha makala tatu kuhusu athari
za lishe ya mama mjamzito kwa afya na ukuaji wa kiakili wa mtoto ambaye
bado hajazaliwa. Wengi wanafahamu kuwa akina mama wajawazito wanapaswa
kula chakula chenye virutubisho vyote vinavyohitajika ili kuhakikisha
kuwa watoto wao watakaowazaa wamerutibika vya kutosha wakati wakiwa
kwenye fuko la uzazi. Hata hivyo, kile ambacho hatukubaliani nacho hivi
sasa ni kwamba chakula cha mama mwenye mimba kinaweza kuwa na taathira
chanya kwa afya ya watoto kwa muda wa miaka mingi, baada ya kuzaliwa.
Hivi sasa imethibitika kuwa kile kinacholiwa na akina mama wakati wa
ujauzito, chakula ambacho kitakuwa kimejumuisha virutubisho vyote
vinavyotakiwa, kinaweza kuwafanya watoto wao watakaozaliwa kuwa werevu
zaidi. Kwani wataalamu wa afya wanasema kuwa hivi sasa wanaweza kuandaa
kizazi kipya cha watoto werevu kwa kula chakula kinachotakikana wakati
wa ujauzito. Akina mama wajawazito ambao katika kipindi cha ujauzito
hawakupata lishe bora isiyo na mada za protini, nishati, madini na
vitamini kwa ujumla huzaa watoto walio na uzito wa chini. Aidha watoto
hao huwa na uwezekano mkubwa wa kukumbuwa na magonjwa ya kisukari katika
kipindi cha utu uzima.
Wapenzi wasikilizaji baada ya kufahamu
umuhimu wa kula lishe bora kwa mama mjamzito na athari zake chanya kwa
mtoto atakayezaliwa, sasa tuangalie hatari ya unywaji pombe kwa
akinamama wajawazito. Watu wengi wanafahamu madhara yanayotokana na
utumiaji wa madawa ya kulevya na ya kawaida pamoja na uvutaji sigara
wakati wa ujauzito, lakini wanawake wengi hawana ufahamu wa kutosha
kuhusu madhara yanayosababishwa na unywaji pombe wakati wa ujauzito.
Utasikia mume au ndugu, jamaa na marafiki wakimshawishi mama mjamzito
kwa maneno kama vile" hebu pata kinywaji, kitakuburidisha, kunywa mvinyo
kidogo tusherehekee mimba yako. Chupa moja haiwezi kukuathiri bali
itakusisimua tu, Hebu tusherehekee sikukuu" n.k. Nadhani wengi tumewahi
kusikia maneno kama haya na ushauri usiofaa ambao hauna faida yoyote
ghairi ya kuandaa madhara kwa mtoto atakayezaliwa.
Athari za pombe kwa mtoto ambaye bado hajazaliwa:
Unywaji
pombe wa aina zozote wakati mama akiwa na mimba huwa na madhara tofauti
kwa mtoto aliye tumboni mwake, kuanzia zile za wastani hadi kubwa.
Kumbuka kuwa mama anapokunywa pombe mtoto naye hunywa pia. Kuna madhara
makuu matatu yanayoweza kumsibu mtoto ambaye bado hajazaliwa iwapo mama
yake alikuwa akinywa pombe wakati wa ujauzito. Mosi, ni kuweko hatari
kubwa ya kutoka mimba au kuzaliwa mtoto kabla ya miezi tisa, pili,
chembe za mwili za mtoto aliye tumboni zinaweza kuathiriwa au anaweza
kuwa na uzito mdogo na kuzaliwa akiwa na ulemavu zaidi ya mmoja., tatu,
chembe za ubongo wa mtoto huyo zinaweza kuharibiwa na pombe na mtoto
kuzaliwa akiwa na matatizo ambayo kitaalamu hujulikana kama Foetal
alcohol syndrome. Miongoni mwa madhara yanayoweza kumpata mtoto ni kama
vile kuzaliwa akiwa na ulemabu wa kimwili na kiakili. Kwa upande wa
kimwili, mtoto huweza kuathiriwa na mtindio wa ubongo au brain
retardation, mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo sana, na uso
wake kuwa na mwanya mkubwa baina ya pua na mdomo. Kwa upande wa macho,
wengine huzaliwa wakiwa na matatizo ya kuona, masikio hushambuliwa na
baadhi ya magonjwa, n.k.. Na tukitazama upande wa ukuaji wa kimaanawi wa
mtoto, kuna mambo kadha wa kadha ambayo mama anaweza kuyafanya ili
kuandaa misingi bora ya kuwa Muislamu mwema. Maimamu watukufu
wametuambia kuwa, mama mjamzito anapasa daima kuwa katika hali ya wudhu.
Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma anapendelea kumuona
mja wake akiwa katika wudhu huku malaika wakimzunguka. Hivyo mama
hushauriwa kujiepusha na kutenda dhambi, kwa sababu jambo hilo litakuwa
na athari ya moja kwa moja kwa shakhsiya ya mtoto. Kwa hivyo ni jambo
lenye umuhimu kwa akina mama kuwaandalia watoto wetu mwanzo mzuri wa
makuzi bora tangu wakiwa tumboni.
Na sasa hebu tuangalie jinsi unene
unavyosababisha hatari kubwa ya saratani ya matiti kwa wanawake.
Wanawake wanaoongezeka uzito kupita kiasi katika utu uzima, wanakabiliwa
na hatari kubwa na ya muda mrefu ya kukumbwa na saratani za matiti.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa, uzito na kansa ya matiti vinaweza
kuwa na uhusiano wa karibu. Utafiti uliofanywa kwa akinamama zaidi ya
elfu 44 nchini Marekani umeonyesha kuwa, kadiri mwanamke anavyozidi
kunenepa, ndivyo anavyozidi kujiweka katika hatari ya kukumbwa na kansa
mbalimbali, tena katika hatua zake zote. Hatari ya saratani ya matiti
imehusishwa na ongezeko la viwango vya hormone ya estrogen na tishu za
mafuta zinazozalisha hormone hiyo. Hivyo basi, akina mama wanashauriwa
kuboresha uzito wa mwili kwa kufuata misingi ya afya katika kipindi
chote cha utu uzima. Je unafahamu kuwa kansa ya matiti inashika nafasi
ya pili kwa kusababisha vifo miongoni mwa wanawake wa Marekani
ikifuatiwa na saratani ya mapafu?
************************
Ni hayo tu kwa leo.
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!