Kila kitu kinapoanza kwenye hii dunia huwa kinaanza sawa na kitu
kingine. Kwa mfano mimea inapoanza kuchipua yote huanza pamoja lakini
utofauti hujitokeza katika kukua kwake kwa kadri siku zinavyokwenda, kwa
mingine kuwa mikubwa sana na mingine midogo ya kawaida.
Pia hata wanyama wengine wanapozaliwa iwe swala au simba wote huzaliwa
wote wakiwa na nguvu sawa lakini utofauti huanza kujitokeza kwa jinsi
wanavyoendelea kukua. Wengine hujikuta wana nguvu zaidi kuliko wengine
na wengine hubaki wanyonge wanyonge.
Halikadhalika linapokuja suala la mafanikio mambo pia huwa yapo hivyo
hivyo. Hii ikiwa na maana kwamba, kila binadamu amezaliwa sawa na
binadamu mwingine. Hakuna binadamu ambaye atasema alikuja duniani akiwa
na mafanikio na mwingine akiwa hana. Wote tulizaliwa tukiwa hatuna kitu.
Kama mambo yako hivi, ni nini kinacholeta tofauti hizi kubwa? Kwa nini
wengine wawe matajiri na wengine wawe maskini? Je, matajiri wanakipi cha
ziada kinachowafanya wafanikiwe? Kimsingi, huwa yapo mambo mengi kidogo
yanayosababisha wengine wawe matajiri na wengine kuwa maskini.
Lakini katika makala haya tutaongelea mambo matatu ambayo yanahusiana na
tabia ambazo zinaleta utofauti kati ya maskini na tajiri. Ni kweli zipo
tabia ambazo matajiri wanazo na huwafanya wao kuwa matajiri kila
kukicha. Ni tabia ambazo huwatenga kabisa na maskini na kuwaacha
matajiri waendelee kufanikiwa.
Ikiwa utaamua kujifunza na kuzifatilia tabia hizi kwa karibu, uwe na
uhakika utajiri utakuwa mikononi mwako muda sio mrefu. Nasema hivyo
nikiwa na maana hii, ukitaka kuwa tajiri fanya yale ambayo matajiri
wanafanya nawe utafanikiwa na kuwa kama wao.
Hebu kwa pamoja bila kupoteza muda, tuangazie nukta kadhaa, zinazoweza
kutuonyesha tabia zinazowatenga kati ya matajiri na maskini.
1. Kuwekeza.
Watu wenye sifa ya utajiri ndani mwao hata kama bado hawajafika huko
kwenye utajiri halisi ni wawekezaji wazuri sana. Si watu wa kuridhika na
chanzo kimoja cha mapato. Wana vitega uchumi vingi sana ambavyo
vinawasaidia kuingiza mapato kwa wingi hata kama wamelala.
Kwa mfano uatakuta wamewekeza kwenye mashamba, mafuta, migodi na maeneo
mengine mengi. Hii ni sifa mojawapo kubwa inawatenga maskini na
matajiri. Ukiona una kitega uchumi kimoja ujue unajizibia nafasi
mwenyewe ya kuelekea kwenye utajiri mkubwa.
2. Kuweka akiba.
Suala la kuweka akiba kwa watu matajiri sio suala la hiari, kwao ni
lazima. Angalau huweka asilimia kumi ya kile wanachokipata. Wanajua
vizuri akiba hizo ni msaada mkubwa kwa baadae katika suala zima la
kuwekeza. Wao katika kuweka akiba ni lazima, na pia hawana mchezo katika
hilo.
Kutona na tabia hii, huwafanya wazidi kufanikiwa kila siku na kuwaacha
maskini wakibaki kuwa maskini. Ni kitu ambacho unatakiwa kujifunza na
kuelewa kwamba, akiba ni jambo la msingi sana kujiwekea kama unataka
kuwa tajiri. Vinginevyo acha kuweka akiba, uendelee kubaki kwenye
umaskini.
3. Kutoa.
Tabia nyingine inayowatenga watu matajiri na maskini ni ile hali ya
kutoa. Watu matajiri ni watoaji wazuri sana wa pesa na mali zao. Hufanya
hivi si kwa sababu wanazo nyingi, bali kutoa ni moja ya kanuni kubwa ya
mafanikio walioamua kuitumia. Huwezi kufanikiwa sana kama hutoi.
Ieleweke hivi, maskini wanaendelea kubaki kuwa maskini kwa sababu ya
uchoyo walionao. Hukumbatia sana walivyonavyo na kusahau kutoa. Kosa
hilo huwafanya wazidi kuendelea kuwa maskini siku zote za maisha yao.
Ili kuwa tajiri ni lazima kutoa.
Kumbuka, tabia ya kuwekeza, kuweka akiba na kutoa ni moja ya tabia kubwa
zinazo watenga matajiri na maskini. Matajiri wanajikuta wakiwa ni watu
wakuzifanyia kazi tabia hizo na kuwafanya kuwa matajiri na maskini
hubaki na umaskini wao kwa sababu ya kutokuzifanyia kazi tabia hizo.
Chukua hatua ya kutenda ili kubadili maisha yako.
SHARE AND COMMENT.............
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!