Mzee Jumbe Ausia Asizikwe Kiserikali:;
“MIMI Aboud Jumbe Mwinyi, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunibariki
kuzaliwa ndani ya Uislamu na namuomba aniruzuku kufa na kufufuliwa ndani
ya Uislamu”.
Hayo ni sehemu ya yaliyomo katika Wasia wa Rais Mstaafu
wa wa Zanzibar Alhaj Aboud Jumbe ambaye hivi sasa ametimiza umri wa
miaka 80.
Akiwa na akili timamu kabisa Mzee Jumbe ameandika wasia huo wiki hii
ambao nakala zake zimesambazwa kwa watu mbalimbali likiwemo gazeti hili.
Wasia
huo wenye kuashiria kutahadharisha juu ya yale yanayoweza kuja kufanywa
kinyume na ridhaa yake, umekuja siku chache baada ya kifo cha Rais
mwingine Mstaafu wa Zanzibar Sheikh Idris Abdul Wakil.
“Ni matumaini yangu kwamba kama Mwenye Enzi Mungu alivyonirehemu kuwa
Muislamu, atanijaalia nikifa kukoshwa, kuvishwa sanda, kutiwa katika
jeneza, kusaliwa na kuzikwa kwa mujibu wa sunna ya Mtume Muhammad
(sa.w.)”, umeagiza wasia huo uliosainiwa kwa niaba
yake na Msaidizi wake Bwana Abubakar.
Agizo hilo linahusisha pia jeneza lake kutofunikwa bendera ya Taifa
au ya CCM, kuwepo na utabaka katika kubeba jeneza na ufukiaji wa kaburi.
Akiwashuhudisha Mufti wa Zanzibar, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Naibu
Kadhi Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Sharrif Juneid, Masheikh wengine na
wanawe, Alhaj Jumbe amesisitiza kuwa kufanyiwa si ombi bali ni haki yake
kama binadamu, kama Muislamu na kama Mtanzania.
Amesema haki ya uhuru wa kuabudu imeelezwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 19 (1) na (2).
Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu mtu anapokufa ni haramu kwa ndugu
au jamaa zake kuomboleza kwa nyimbo, kunyoa vipara, kuvaa vitambaa au
nguo nyeusi wala kulia kupita kiasi.
Aidha, imesuniwa kuwafariji (taa’zia) wafiwa kwa muda wa siku mbili tu.
“Atta’azia marrataan” ameagiza Mtume (s.a.w) akiwa maana ya kuwafariji wafiwa ni mara (siku) mbili.
Katika wasia wake Alhaj Jumbe amesema maana ya kuumbwa mauti na uhai
sababu na lengo lake ni kuwafanyia wanaadamu mtihani kupimwa miongoni
mwao mwenye vitendo vizuri.
“Nikiwa hai, dhamana ya vitendo vyangu
inaniangukia mimi mwenyewe, nikifa dhamana ikiwa vitendo vyema au vibaya
nitakavyofanyiwa itawaangukia waandalizi, watendaji na wenye kushiriki
katika vitendo hivyo”, amesisitiza mzee huyo aliyekuwa pia Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akimshudisha Mwenyezi Mungu katika wasia huo amekataa maziko yake kufanywa kinyume na taratibu za Kiislamu.
“Sitaki bendi, sitaki mizinga, sitaki maombolezo wala lolote lingine
lenye hata chembe ya kufuru”, ameandika kwa mkazo mzee huyo.
Aidha, amewaapiza kwa kumshuhudia Mwenyezi Mungu wale watakaojaribu kufanya kinyume na anavyoagiza.
“Sitaki hivyo nikiwa hai, nitakapoondoka katika dunia Mwenye Enzi
Mungu anatosheka kuwa shahidi wangu, duniani na akhera”, mzee Jumbe
amemaliza wasia wake alioutanguliza aya ya Qur’an isemayo “Enyi wenye
kuamini, mcheni Mwenyezi Mungu vile ipasavyo waja kumcha, wala msife ila
Ilhali ni miongoni mwa Waislamu. (3:101)
—
Chanzo: islamtanzania.org
webmaster@islamtanzania.org
Jamii Forums
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!