
BAADHI ya viongozi wa dini na wasomi, wamempongeza Rais mstaafu wa Awamu
ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa hatua yake ya kuwakutanisha Rais John
Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Wamesisitiza kuwa hatua hiyo, inaonesha jinsi ambavyo demokrasia na
amani imekomaa nchini. Viongozi hao walikutana juzi katika Misa Takatifu
ya kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya ndoa ya Rais mstaafu Mkapa na
mkewe, Anna, iliyofanyika juzi kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro
Oysterbay, Dar es Salaam.
Viongozi wa dini waliozungumza na gazeti hili na kupongeza hatua hiyo ni
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba la Kanisa Katoliki, Mhashamu
Methodius Kilaini, Askofu wa Kanisa la Good News for All Ministry, Dk
Charles Gadi na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum.
Kwa upande wa wasomi, gazeti hili lilizungumza na wahadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana na Profesa Kitila Mkumbo ambaye
pia ni Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo. Mwingine ni Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa
Mwesiga Baregu.
Maoni ya viongozi wa dini Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya
simu, Askofu Kilaini alisema jambo walilolifanya viongozi hao ni la
kuungwa mkono na Watanzania wote.
“Jambo hili tumeliona na tumelifurahia sana na inatupa funzo kwamba
tunapofanya siasa, tusisahau utu wetu. Siasa tuiache kama siasa… pia
tumejifunza kwamba siasa si uhasama kwa sababu viongozi hawa wameweza
kukutana na kupeana mikono,” alisema.
Alisema; “Mtu unapopeana mkono na mtu na kuangaliana usoni inaonesha
kwamba hakuna uadui kati yenu hivyo kwa viongozi hao wameonesha kwamba
wanakinzana katika siasa tu...” alisema.
Askofu Kilaini alisema, wanaamini kwamba kukutana kwa viongozi hao ambao
wana mrengo tofauti ni mwanzo mzuri wa maridhiano ya pande zote mbili
ambazo zimekuwa na misuguano ya kisiasa.
“Nawashauri Watanzania wenzangu kwamba kama viongozi wetu wakuu wameweza
kukutana na kupeana mikono na kusalimiana tena na kupiga picha ya
pamoja wakiwa karibu basi na sisi wafuasi wao tusijengeane chuki bali
tupendane… tusiendelee kusigana na kupigana maana viongozi wetu wenyewe
wanaelewana ila wanatofautiana tu katika siasa,” alisema.
Kwa upande wake, Askofu Gadi alisema kwa viongozi hao kukutana wanaamini
kwamba maombi wanayoyafanya yanazidi kuimarisha umoja, amani na
mshikamano wa nchi.
“Watanzania tuzidishe maombi maana yana nguvu na kupitia maombi hata
yasiyowezekana yanawezekana, viongozi wa dini tuombe sana na tuhamasishe
watu waombe maana hata hawa viongozi wetu ni waumini wetu na ni
washiriki wazuri wa nyumba za ibada na tunashika nafsi zao,” alisema.
Aidha alisema viongozi hao wameonesha kwamba ni watu wanaomuogopa na
kumheshimu Mungu kwa kusalimiana kwa upendo na kusisitiza kwamba maombi
huleta upatanisho na kubadilisha jamii.
Alisema kupitia kanisa hilo, wamekuwa wakifanya huduma ya maombi mara
kwa mara ambapo kwa sasa wameanza maombi ya siku 1,001 na wiki iliyopita
walifanya maombi wilayani Chato mkoa wa Geita kwa ajili ya kumuombea
Rais Magufuli katika utendaji wake.
Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa alisema tukio hilo ni
la heri, kwa kuwa watu walikuwa wakiwatazama viongozi hao kama maadui,
hivyo kwa kupeana mikono wameithibitishia jamii kwamba wanatofautiana tu
katika siasa.
“Walichokifanya viongozi wetu wameonesha kwamba, siasa si uadui na
tunaomba kukutana huko kuwe heri na waendelee kukutana mara kwa mara kwa
ustawi wa Taifa letu,” alisema.
Wasomi nao wafunguka Katika hatua nyingine, wasomi nao walieleza
kupongeza kitendo hicho kilichowakutanisha walikuwa wapinzani wa karibu
wakati wakigombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Magufuli na
Lowassa.
Kwa namna ya pekee wasomi hao walipongeza pia kitendo hicho cha
kizalendo, ambacho viongozi hao walikionesha kwa kushikana mikono,
kutabasamu na kuonekana wakiteta kwa nyuso za tabasamu.
Profesa Baregu mbali na kupongeza uzalendo huo, alisema kukutana na
kuzungumza kwa Rais Magufuli na Lowassa ichukuliwe kuwa ni fursa kwa
viongozi hao, ambayo wanapaswa kuitumia kufanya mazungumzo ya kuimarisha
amani.
“Hiyo itafsiriwe kuwa ni fursa ambazo huwa inajitokeza katika mazingira
tofauti, aidha kwa kupangwa au bila kupangwa, lakini kikubwa watumie
fursa hiyo vilivyo,” alisema Profesa Baregu. Alisema kukutana kwa Rais
Magufuli na Lowassa ni fursa nzuri kwani walikuwa hawajawahi kukutana
tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba, mwaka jana.
Alisema mambo machache ambayo viongozi hao walizungumza juzi katika muda
mfupi, yataweza kutumika vizuri kutatua mambo ya kisiasa ambayo
yanaendelea hapa nchini kwa sasa na kufungua njia nzuri.
“Na hii inaweza kuwa njia nzuri kuzungumzia masuala ya kisiasa,
demokrasia na pia Katiba mpya ambayo ndio kilio kikubwa cha Watanzania
ili tuweze kupata Katiba mpya,” alisema Profesa Baregu.
Msomi huyo alisema pia fursa hiyo itumike kuleta amani kwa wananchi na
kwa maana ya kupatikana maridhiano katika masuala ya kisiasa.
Profesa Mkumbo alimpongeza Mkapa kwa kitendo hicho cha kuwakutanisha
viongozi hao na pia kuwapongeza Rais Magufuli na Lowassa kwamba pamoja
na walikuwa katika mchuano mkali katika Uchaguzi Mkuu uliopita na mwisho
Rais Magufuli kupata ushindi, lakini wameonesha bashasha ya aina yake.
“Huo ndio utanzania ambao Watanzania wanautaka, tunaweza kutofautiana
bila kugombana, utanzania wetu haujali dini, kabila wala kitu kingine
chochote,” alisema Profesa Mkumbo.
Aidha alisema muonekano pia wa viongozi hao wawili, ulionesha wazi
walikuwa katika hali ya amani, “hata muonekano wao uliweza kuona kabisa
ilikuwa safi, na Rais wetu kama tunavyomjua si mtu wa kuficha jambo
lakini walicheka na kuzungumza vizuri.”
Kwa upande wake, Dk Bana alisema kwa muonekano ambao walionesha viongozi
hao wawili jana ilionesha changamoto za kisiasa zilizokuwepo,
hazitaendelea kuwepo tena kwani viongozi hao walionekana kuteta kwa
upendo.
“Ile inaonesha kabisa harakati za Ukuta (Umoja wa Kupambana na
‘Udikteta’ Tanzania) hazipo tena na jana (akimaanisha juzi) zilizikwa
pale, walionekana kunong’ona na kupeana mikono kwa amani kabisa na
inaonesha wote ni wamoja katika kujenga nchi yenye amani,” alisema Dk
Bana.
Alisema nasaha ambazo zilitolewa pia viongozi wa dini katika hafla ile,
zitumike pia vizuri katika kuondoa masuala yote ya kisiasa, ambayo
yamekuwa yakileta mvutano na badala yake kujenga upendo na amani.
Alisema uwazi wa Rais Magufuli na maneno aliyozungumza, yalikuwa ya
busara.
COMMENT AND SHARE................................
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!