Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika
kipindi chenu hiki cha Ijue Afya Yako. Wiki iliyopita tulieleza kwa
urefu kuhusu ugonjwa wa figo na kufafanua jinsi mtu anavyoweza kuugua
ugojwa huo. Wiki hii pamoja na mambo mengine tutaeleza jinsi ugonjwa huo
unavyoweza kutibika. Basi msiondoke kando ya redio zenu ili muweze
kufahamu namna ya kutibu ugonjwa huo.
&&&&&&&&
Tulisema kwamba dalili ya
kwanza ya kuugua ugonjwa wa figo ni kupungua kwa kiasi cha mkojo. Dalili
nyingine ni maji kujaa mwilini, madini za mwili kuwa juu hasa ya
potasiamu, asidi nyingi, na mgonjwa kujisikia au kuwa na matatizo katika
moyo na anaweza pia kuwa na matatizo katika ubongo. Mgonjwa pia anaweza
kukosa hamu ya kula chakula chochote na hali hiyo kumfanya au
kusababisha adhoofike mwili. Nyongeza za dalili za mtu kuugua ugonjwa wa
figo hasa kwa wale wagonjwa ambao hawagunduliki mapema ni kuvimba macho
mara tu baada ya kuamka wakati wa asubuhi na uvimbe kupungua baadaye.
Dalili kubwa nyingine ni mgonjwa kupungukiwa na damu mwilini.
Tiba ya figo
Mojawapo
ya njia za matibabu ya figo ni kukisaidia kiungo hicho kufanya kazi
kama kawaida kwa kutumia mashine za kitiba kunakojulikana kama dialysis.
Dialysis ni usafishaji wa figo unaohusiana na utoaji wa maji yaliyojaa
mwilini, uchafu, pia sumu zinazotokana na vyakula au dawa. Tiba ya
'dialysis' ni ya gharama kubwa kwa kuwa kila mgonjwa anapohitaji
kuipata, hutakiwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha huku akitakiwa kuipata
tiba hiyo mara nyingine hata mara tatu kwa wiki. Kwa mfano nchini
Tanzania mwenye matatizo ya figo huhitaji shilingi laki 3 kila wiki kwa
ajili ya tiba hiyo ambayo hufanyika mara tatu hadi nne kwa mwezi.
Mgonjwa akifikia hali inayohitajia matibabu haya, huhitaji huduma hii ya
kusafishwa damu kwa mashine kwa umri wake wote, kama hatopandikizwa
figo nyingine. Dialysis ni mchakato wa kutoa maji yasiyohitajika kutoka
kwenye damu, mchakato unaofanywa kwa mashine maalumu zinazounganishwa
kwa mgonjwa baada ya figo kushindwa kufanya kazi. Hii ni kwa sababu ni
lazima damu isafishwe na kuondolewa taka hizo zilizoingia kwenye mfumo
wa damu kwani zikibakia huhatarisha maisha. Kwa kawaida figo hufanya
kazi ya kuchuja uchafu katika mwili, lakini baadhi ya wakati figo
hushindwa kufanya kazi yake hiyo muhimu kutokana na sababu mbalimbali
tulizozizungumzia huko nyuma. Usafishaji wa figo hufanyiwa wagonjwa
ambao figo zao zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na maradhi ambapo tiba
hiyo huwa ni ya dharura.
&&&&&&&&&&&
Wakati wa
kufanyiwa tiba ya dialysis mgonjwa hutundikiwa mipira maalumu, huku
kwenye mashine kukiwa na figo ya bandia ambayo kazi yake ni kupitisha
damu, kuisafisha na kuirudisha mwilini. Kwenye mashine maalumu
kunakuwepo na mipira kadhaa ikiwemo ya kupitishia damu kupeleka kwenye
figo bandia inayofanya kazi kama ya mwilini, na mirija mingine ambayo ni
mikubwa kiasi inayotumika kutoa maji yasiyohitajika mwilini na sumu,
huku mingine ikitumika kurudisha damu safi mwilini. Mgonjwa hulala
kitandani wakati wa kufanyiwa tiba hii kwa masaa manne, bila kuchomwa
sindano ya usingizi, kwa kuwa dialysis haina maumivu makali. Vilevile
mgonjwa hutobolewa eneo maalumu mwilini kwa ajili ya kupitishia mipira,
kuna wanaotobolewa shingoni au mkononi kulingana na anavyotaka mgonjwa.
Hata hivyo, tiba hii licha ya kuwa na gharama kubwa ambazo wagonjwa
wengi huwa hawazimudu hasa katika nchi masikini, haina uhakika wa
kupunguza tatizo kwa asilimia 100, bali kwa asilimia 40 hadi 50 pekee.
Suala hili linasisitiza umuhimu wa kuzitunza vyema figo zetu na
kujiepusha na mambo yanayosababisha figo kuharibika. Sio vibaya ukijua
mpenzi msikiliza kuwa, mwili wa binadamu una uwezo wa kumudu kazi zake
kwa kutumia figo moja tu, licha ya mwanadamu kuumbwa na figo mbili. Hii
ndio sababu mtu huanza kuhisi matatizo ya figo pale inapokua figo zote
mbili zimeshindwa kufanya kazi na kuharibika. Na pia ndio sababu watu
wanaweza kusaidia wagonjwa figo moja na kubakia wakiishi kwa kutumia
figo moja iliyobakia bila matatizo yoyote.
Tiba nyingine ya ugonjwa
huu ni ya kupandikiza figo inayojulikana kitaalamu kama kidney
transplant. Tiba hii hufanywa hasa kwa mgonjwa ambaye figo yake imekufa
na haiwezi kufanya kazi kwa msaada wa dialysis ambapo hupandikizwa au
kuitikwa figo ya mtu mwingine mwilini mwake. Tiba hii ya figo ina
gharama kubwa sana na ni ngumu kufanyika hasa kwa kuzingatia kuwa figo
inayotakiwa kupandikizwa mgonjwa hutoka kwa mtu mwingine. Pia ni vigumu
kupatikana mtu atakayejitolea figo yake na abakiwe na figo moja, na hata
akipatikana baadhi ya wakati huwa hailingani au haiendani na figo ya
mgonjwa suala ambalo hupekekea kufanyika tiba hiyo kuwa kugumu na
mafanikio yake kuwa madogo. Pia tiba hiyo huwa na madhara kiafya hasa
kwa walio kwenye hatua ya tano ya tiba hiyo. Madhara hayo ni pamoja na
maradhi ya moyo, miguu kukaza na maumivu ya kifua.
&&&&&&&
Wapenzi wasikilizaji, miongoni
mwa sababu zinazodhuru figo baadhi huweza kuepukika. Miongoni mwa mambo
yanayosababisha figo kuharibika ni ulevi, kuvuta sigara na matumizi
holela ya dawa za maumivu. Kwa ajili hiyo jamii inashauriwa kuepuka
kunywa pombe, kuvuta sigara na kutumia hovyo dawa za maumivu. Pia
tunashauriwa kufanya uchunguzi wa miili yetu mara kwa mara au kwa ibara
ya kitaalamu check-up, na pale tunapobaini figo zetu zimeanza kuathirika
basi tuanze matibabu mapema na kuzuia kuharibika kabisa viungo hivyo
muhimu mwilini. Pia tunashauriwa tuonapoona dalili tulizozitaja
kuhusiana na ugonjwa wa figo basi haraka twende hospitali au tukamuone
daktari.
&&&&&&&&&&&&&&&&&
Tunakiendeleza
kipindi chetu kwa kutoa ushauri wa lishe na ulaji kwa watu mwenye
ugonjwa wa figo. Ulaji wa mtu mwenye ugonjwa huu unapaswa kudhibitiwa
kwa kiasi kikubwa kwani figo huwa haziwezi tena kutoa mabaki ya protini,
maji, chumvi na potassium kwa urahisi vinapozidi mwilini. Vyakula
vyenye chumvi na potassium nyingi viepukwe ikiwa ni pamoja na kuzingatia
mambo yafuatayo:
Kupunguza kiasi cha nishati-lishe au calories.
Kiasi cha nishati-lishe na protini kinapozidi mwilini huzipatia figo
ambazo zimeathirika kazi kubwa. Pia kupunguza kiasi cha vinywaji au
vimiminika, ili kupunguza kujaa kwa maji mwilini ambako husababishwa na
kushindwa kwa figo kutoa maji mwilini. Maji yakizidi mwilini husababisha
kushindwa kupumua, shinikizo kubwa la damu, kuvimba mwili na huweza
kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi.
Pia mtu mwenye matatizo ya
figo anapaswa kupunguza kiasi cha sodium au chumvi anayokula. Kiasi cha
maji mwilini hudhibitiwa na sodium na pale madini hiyo inapozidi mwilini
husababisha maji kubakia mwilini. Hali hii huweza kusababisha ongezeko
la uzito ghafla, kuvimba kwa viungo vya mwili, shinikizo kubwa la damu,
kushindwa kupumua na hatimaye kusababisha ugonjwa wa moyo. Vyakula
vyenye sodium kwa wingi ni vyakula vilivyosindikiwa kwa chumvi kama
nyama, samaki na soseji za makopo. Mgonjwa anapaswa kujenga tabia ya
kutoongeza chumvi kwenye chakula wakati wa kula. Vilevile anapaswa
kupunguza kiasi cha potassium katika mlo wake. Madini ya potassium
yanapozidi mwilini husababisha misuli kuwa dhaifu na mapigo ya moyo
kubadilika na yakizidi sana huweza kusababisha kifo cha ghafla. Ni
muhimu kudhibiti kiasi cha potassium kwa ukaribu. Vyakula vyenye
potassium kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maparachichi, ndizi mbivu,
maboga, machungwa, peach, peasi, matunda yaliyokaushwa na maharagwe.
Vyakula vyenye potassium kwa kiasi kidogo ni pamoja na zabibu, machenza,
mahindi mabichi, cauliflower, na matango. Unaweza kupunguza kiasi cha
potassium kwenye chakula kwa kuchemsha na kumwaga maji ya ziada.
Pia
mgonjwa wa figo anapaswa kupunguza kiasi cha phosphorus. Uwiano wa
calcium na phosphorus mwilini ni muhimu kuwezesha afya njema ya mifupa,
misuli na neva. Phosphorus inapozidi mwilini mifupa huwa myepesi na
rahisi kuvunjika suala linatokana na mwili kushindwa kuhifadhi na kuitoa
calcium kwenye mifupa. Vyakula ambavyo vina phosphorus kwa wingi ni
pamoja na maziwa na vyakula vya jamii ya maziwa, nyama, shellfish,
vyakula ambavyo havijakobolewa, maharage, karanga, korosho na chokoleti.
Wagonjwa wa figo pia huhitaji vitamini na madini ya nyongeza kutokana
na kutokula aina mbalimbali za vyakula na hivyo kuweza kusababisha
upungufu wa baadhi ya virutubishi. Damu inapochujwa kwa njia ya dialysis
pia huondoa vitamini kwenye damu kwa hivyo vitamin hizo ambazo ni
dharura kwa mwili hupaswa kufidiwa kwa kula virutubishi vya nyongeza au
supplements. Virutubishi vya nyongeza vinapaswa kutolewa kwa mgonjwa wa
figo baada ya ushauri wa daktari.
&&&&&&&&&
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!