NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Dkt Hamis Kigwangalla amesema wanachama wa Yanga wanapaswa kulaumiwa kwa
kutomtendea haki mwenyekiti wao Yusuf Manji, baada ya kushindwa
kumuuliza maswali.
Kauli hiyo ya Kigwangala imekuja siku chache baada ya mkutano mkuu wa
dharura wa Yanga kukubali kumkodisha Manji timu yao kwa miaka 10.
Akizungumza juzi baada ya mchezo wa kirafiki kati ya Simba na AFC
Leopard, Dkt Kigwangalla alisema wanachama hawakumtendea haki kwani
walipaswa kumuuliza Manji maswali ambayo yangetoa mustakabali wa klabu
yao.
“Manji anapaswa kuweka wazi ni kwa nini apewe asilimia 75 na sio 25
ya faida itakayopatikana na ni kwa nini atake kukodishwa miaka 10 na si
miwili au mitatu na kwa gharama gani?”Alihoji. “Naona mwanga kwa upande
wa Simba ambayo inaenda kwa mfumo wa Kampuni na kuuza hisa, ila
ninachowashauri Mo Dewji (Mohamed) apewe asilimia 40 na si asilimia
51,hii itapunguza kumfanya atoe maamuzi yake peke yake. “
Asilimia zilizobaki ziende kwa wanachama ili nguvu ibaki kwa watu wengi zaidi na si mtu mmoja awe na nguvu.
“Siwaungi mkono Yanga hata kidogo, kumpa mtu mmoja timu kwa miaka 10
bure, nafurahi wanavyofarakana kwa vile mimi ni shabiki wa Simba, waache
wavurugane sisi tunaelekea kwenye mafanikio. “Manji amekuwa na sauti
Yanga kuliko mtu yeyote, amewashika masikio anachotaka yeye ndio hicho
hicho, ana sauti kuliko mtu yeyote, anafukuza watu, anafanya anavyotaka,
hii si sawa,” alisema Dkt Kigwangalla.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipoombwa
kutoa maoni yake juu ya hilo alisema: “Unataka kujua kwa nini Tanzania
ni masikini pamoja na utajiri mkubwa wa maliasili tulizonazo? Soma
mkataba wa Yanga wanaosaini”.
Hata hivyo, Mjumbe wa Bodi ya wadhamini wa klabu hiyo, Francis
Kifukwe alisema wao sio wajinga wakubali kumpa Manji timu miaka 10 bila
kufuata mambo ya msingi na kwamba kuna mambo mengi watayafuatilia na
kutoa tamko siku yoyote kuanzia leo.
Habari ambazo HabariLeo imezipata zinasema kuwa bodi ya wadhamini ilitarajiwa kukutana jana kupitia maombi ya Manji.
“Baraza litapitia kipengele kimoja baada ya kingine kuangalia klabu
itakavyonufaika, vigezo vitakavyotumika katika kumkodisha, kabla ya
kuridhia ombi la Manji,” alisema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!