
MWACHENI Jose Mourinho na kiburi chake aisee. Ungeweza kudhani angetoa
maneno ya kufariji kwa kinda Marcus Rashford baada ya juzi kuibuka na
ushujaa wa dakika za mwisho katika pambano gumu dhidi ya Hull City
ugenini. Mourinho bado hajalainika kirahisi hivyo.
Rashford alitokea katika benchi akichukua nafasi ya Juan Mata katika
dakika za mwisho za pambano hilo la kusisimua lililopigwa Uwanja wa KCOM
jijini Hull na dakika chache baadaye akaifungia Man United bao la
ushindi.
Rashford bado hajaanza mechi yoyote chini ya Mourinho licha ya kutamba
katika msimu uliopita akiwa na Kocha aliyetimuliwa, Louis van Gaal kiasi
cha kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England kilichoshiriki
michuano ya Euro nchini Ufaransa.
Kwa sasa ametoswa na kocha mpya wa England, Sam Allardayce kwa sababu
hiyo hiyo ya kutochezeshwa na Mourinho huku akimpeleka katika kikosi cha
timu ya taifa ya England chini ya umri wa miaka 21.
Hata hivyo, licha ya kufunga bao muhimu jana, Mourinho amedai kwamba bao
hilo halijamshawishi kuanza kumpanga Rashford tangu mwanzo kwa sababu
inabidi afanye kazi kwani, wachezaji wanaoanza wamekuwa wakifanya kazi
nzuri.
“Sio kwa sababu amekuwa mshindi wa mechi basi nitabadili mawazo. Huwezi
kutompanga mchezaji mwingine wakati wanaoanza wanacheza vizuri.
Mshambuliaji wetu namba moja (Zlatan Ibrahimovic) ni mchezaji hatari. Si
tu kwamba ni mfungaji lakini anacheza vyema kitimu.
Anatengeneza nafasi,” alisema Mourinho.
“Ni kweli tunaweza kuanza na mchezaji mwingine mbele ya Zlatan lakini
inabidi utawale sana uwanjani ili ulingane naye. Rashford anaweza
kucheza au kukaa katika benchi. Hata hivyo, atacheza mechi nyingi msimu
huu. Najua alikuwa mzuri msimu uliopita na sasa nafanya naye kazi kila
siku na nafikiria hivyo. Alitupa mbinu tofauti alivyoingia.”
Mourinho alikiri kwamba timu yake ilikuwa imeshinda katika dakika za Sir
Alex Ferguson, lakini aliamini kuwa bao lilikuwa njiani linakuja huku
pia akiipigia saluti safu ya ulinzi ya Hull City ambayo ilicheza kwa
ushirikiano mkubwa ndani ya dakika 90 mpaka Rashford alipofunga bao la
ushindi kwa krosi fupi ya Wayne Rooney.
“Sir Alex Ferguson ni mtu anayeheshimika katika klabu hii na nina furaha
kusema kwamba tulishinda katika muda wa Fergie. Nina furaha sana kusema
hivyo,” alisema Mourinho ambaye anajulikana kwa tabia yake ya
kumheshimu kocha huyo mkongwe wa Scotland.
“Najua tunapofunga mwishoni watu watasema kuna bahati kidogo lakini
ukweli ni kwamba tulistahili, sana sana katika kipindi cha pili.
Tulitawala sana mechi, tulicheza kwa nguvu kasi tukishambulia na
niliamini kuwa bao lingekuja tu,” alisema Mourinho.
“Inabidi niseme kwamba Hull City walifanya kazi ya ajabu na walijilinda
sana kwa kila namna. Hawakuweza kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwa
sababu naamini tulijilinda vizuri sana. Hongera kwao na kama ningekuwa
Mwenyekiti wao ningempa kazi ya kudumu kocha Mike Phelan haraka sana.”
“Kila mtu anaona kwa macho yake, wachezaji wanatoa kila walichonacho kwa
ajili yake. Wasingeweza kufanya zaidi ya kile walichofanya na hongera
sana kwa Mike na vijana wake,” alisema Mourinho ambaye kwa ushindi huo
United yake inakuwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu za
mwanzo dhidi ya Southampton, Bournemouth na Hull City juzi usiku.
Hata hivyo, mtihani wa kwanza halisi kwa United unatazamiwa kuwa dhidi
ya Manchester City katika pambano lijalo la Ligi Kuu baada ya mechi za
kimataifa zinazotazamiwa kuchezwa wikiendi ijayo.
Pambano hilo litachezwa Septemba 10 huku likitazamiwa kuwakutanisha
makocha wawili mahasimu wa muda mrefu, Jose Mourinho na Pep Guardiola wa
Manchester City.
COMMENT AND SHARE...................................
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!