JINSI YA KUKUZA NA KUTANUA BIASHARA YAKO NDOGO.
Habari.
Toleo hili ni mahususi kwako wewe kama, ni mfanyabiashara ndogondogo, au
ni mfanyabiashara mkubwa na ungependa kukua zaidi, au kama wewe una nia
ya dhati ya kuanzisha na kuendeleza biashara yoyote inayokidhi misingi
ya haki na sheria za nchi.
Karibu. Kama mfanyabiashara siku zote unatizama katika upande bora
zaidi, upande wa maendeleo. Hii ina maana siku zote unapenda kuiona
biashara yako ikikua na kupanuka zaidi, unaweza kuwahudumia wateja wengi
zaidi na faida inazidi kuongezeka.
Haya ni mambo 5 ya msingi kama una nia ya kukuza biashara yako hasa
katika nchi za Afrika Mashariki. Ni muhimu kutambua kwamba jirani yako
kabisa Mama Jofre au yule msukukuma guta anayetumia bidhaa zako ndiye
atakayekukuza wewe. Biashara huanza kutanuka kuanzia chini kabisa
nikimaanisha kwamba mteja aliye karibu na biashara yako ndiye anayeweza
kusema mema kuhusu biashara yako akaaminika zaidi kuliko tangazo lako
lililogharimu zaidi ya milioni mbili kuruka hewani.
1.
Katika biashara hasa ndogondogo ni muhimu kufahamu soko lako liko wapi
na kama bidhaa yako inaweza kujiuza. Utakapogundua ni wapi soko lako
lilipo anzia hapo, ongeza juhudi, ubunifu na ustadi wa huduma. Kwa mfano
muuza senene kutoka Kagera unapogundua kwamba watu waishio Dar es
Salaam ndio hununua zaidi biashara yako, wapelekee huduma, jenga mabanda
Dar es salaam
au ongeza idadi ya vijana wanaotembeza biashara yako. Fuatilia ni aina
gani ya senene wanaopendwa zaidi, Je, ni wale wenye pilipili au wenye
iriki au wale wenye pilipili na iriki pamoja. Fuatilia je, ni wale
waliokauka sana au kiasi. Ukishagudua ni wapi wanaouza zaidi, ongeza
mzigo wako. Watengeneze kama soko lako linavyowahitaji kisha ingiza
sokoni, utauza na ukiuza utapata pesa zaidi.
2. Jambo la pili ni jinsi ya kutumia pesa baada ya kupata pesa
zaidi.Wengi huadaika na kuwa na pesa nyingi katika wallet, M-PESA,
Airtel Money au Tigo Pesa zao. Usiende baa kuwazungushia marafiki zako
raundi kisa pesa imepatikana nyingi zaidi ya ile uliyoitarajia.
Simaanishi kwamba usifurahi na wenzako au ujitenge na rafiki zako, La
Hasha! Fanya kwa kiasi kidogo sana. Kwa nini ninasema kiasi kidogo sana?
Bila shaka wewe bado ni mdogo sana katika biashara. Hivyo unahitaji
kila senti unayoweza kuitengeneza katika kukuza biashara yako. Usipende
starehe sana. Usipende kutumia pesa ili kuonesha kwamba una pesa. Badala
yake wekeza pesa hiyo katika bishara yako hiyohiyo na utaona jinsi pesa
iatakavyozidi kuongezeka. Kama unauza chipsi, gunia moja limemalizika
na umefanikiwa kupata pesa zaidi usitake kununua gunia moja tena.
Jiwekee deni sasa ununue magunia mawili. Yakimalizika pesa itakua nyingi
zaidi, usitatake kununua magunia mawili tena jiwekee malengo ya kununua
magunia matatu. Kwa jinsi hii biashara yako itaanza kukua, utapata
wateja zaidi.
3. Jambo la tatu ni kuwa mkweli na muwazi. Siku zote msema uongo
ni mpenzi wa shetani, na wapenzi wa shetani, wow! hawafanikiwi na ni
wabaya. Usipende kutoa sababu zisizo za msingi katika biashara yako. Kwa
mfano, kama una biashara ya mama n'tilie usiwalishe wateja mchuzi
uliobaki jana na kisha wakilalamika ukasema kwamba tatizo limetokea
katika bucha ya nyama.
Lakini zaidi lipa kodi kama bishara yako inahitajika kulipia kodi. Ukiwa
muwazi kwa mamlaka ya kodi huweza kukusikiliza na kukusamehe kodi
kiroho safi tu hasa kama biashara yako ni ndogo. Lakini ukianza kuleta
uongo, mara ukiwaona TRA unafunga duka, au unajificha kabatini ukisikia
hodi ya mama mwenye pango biashara yako itayumba na hautaweza kupanuka.
Isajili biashara yako na hii itakusaidia sana mbeleni.
4. Jambo la nne ni kujitanua kwa kukuza network, kujuana na watu,
kuungana na bishara nyingine katika kutoa huduma zako. Jaribu kuwafanya
watu wengi zaidi wakufahamu. Ziko njia nyingi sana za kufanya hivi
lakini moja ni kuwa na mahusiano mazuri na wafanyabisahara wenzako. Kama
Bwana Juma na Bwana Zengwe ni wafanyabishara wenye mahusiano mazuri
lakini wanamiliki biashara tofauti, mteja akienda kwa Bwana Juma
kuulizia huduma au bidhaa fulani akakosa, ni rahisi kwa Bwana Juma
kumuelekeza mteja huyo moja kwa moja hadi kwa rafiki yake Bwana Zengwe
ambaye yuko na bidhaa au huduma hiyo. Hivyo ni muhimu sana kukuza
mtandao wako katika kila wilaya angalau ujulikane hii itakuwia rahisi
hata kutanua wigo wa soko lako. Lakini pia kama wewe unauza mabati ni
vizuri ukaungana na mfanyabiashara anayeuza cement na pamoja mnaweza
kuunda biashara ya mabati na cement hivyo kuwavutia wateja wengi zaidi.
5. Jambo la tano ni kujaribu kuteka biashara nyingine na kufanya
juhudi ya kupata tenda za serikali. Hauwezi kushinda tenda za serikali
kama haujasajili biashara yako. Lakini hakika kama utaweza kupata tenda
za serikali basi biashara yako itapanuka kwani tenda hizi huhitaji
bidhaa nyingi sana hivyo pesa nyingi pia lakini serikali ni mteja mzuri
sana. Kama umeweza kufanya biashara na serikali hata ya kuwauzia kuni
tu, utashindwa kufanya biashara na nani? Jambo jingine ni kujaribu
kuanzisha biashara nyingine. Kwa mfano kama umeanza na biashara ya
kubrashi viatu, sio vibaya unapokuza mtaji wa viatu ukaanzisha biashara
nyingine ya kuuza malapa, viatu, mikanda au soksi. Hii itakupa mwanya wa
kutegemea zaidi ya biashara moja katika kujipatia mapato yako. Hivyo
itakuza biashara yako.
Kama unavyofahamu biashara inahusisha kujaribu na kuwa tayari kwa hasara
na faida. Lakini biashara sio mchezo wa bahati nasibu kwamba ukipata
umepata, ukikosa umekosa. Hata ukipata ni muhimu kujidhatiti zaidi ili
uzidi kukua na kama ukikosa hata siku moja usije kukata tamaa. Endelea
kupambana na kama ukifuata njia sahihi za kutoa huduma hata siku moja
hautashindwa lazima iko siku biashara itajibu na utaendelea kupanuka
zaidi. Watu wote waliofanikiwa wamewahi kupitia vipindi vigumu, kampuni
ya vifaa vya elektroniki ya Apple, iliwahi kufikia hatua ya kuuza baadhi
ya haki na viwanda vyake ili iepuke kufirisika kabisa. Apple iliamua
kubadili uongozi wake na kupunguza kazi wafanyakazi wengi sana, lakini
kwa kichache Apple ilichobakia nacho chini ya mfanyabiashara wa kuigwa
Steve Jobs, waliweza kuanza upya na mpaka sasa mafanikio yake wote
yunajionea.
Kuwa mbunifu, Kuwa mkweli na Ogopa hasara.
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!