Huu ndio Utofauti Kati ya Diamond na Kiba:;
KUNA vita ya maneno kati ya makundi mawili ya mashabiki wa Muziki wa
Bongo Fleva, wanaowashabikia wasanii Alikiba na Nasibu Abdul ‘Diamond’,
kila upande ukidai mtu wao ndiye anajua zaidi kuliko mwingine.
Ni mjadala mpana katika mitandao ya kijamii, mitaani na hata miongoni
mwa wasanii wenyewe ambao kwa kificho au waziwazi, wamewahi kuzungumzia
nani mkali katika wawili hao ambao wote ni vijana wenye asili ya Kigoma.
Alikiba ama King Kiba, ndiye wa kwanza kuingia na kupata jina katika
Muziki wa Bongo Fleva, katikati ya miaka ya 2000 akiwa na singo yake ya
kwanza, Cinderella ndiyo ilimfungulia milango, kwani alichomoza hadi juu
ambako alidumu kwa muda mrefu.
Huenda Diamond amewahi kuimba kwa kuiga baadhi ya nyimbo za Alikiba, kwa
sababu yeye alianza kupata jina mwaka 2009, mwaka ambao mwenzake tayari
alishakuwa na albamu mtaani.
Unapotaka kufanya ulinganisho wa wawili hawa ni lazima uchague unataka
kuwalinganisha nini, vinginevyo unaweza kujikuta umewekeza katika chuki
au ushabiki, kitu ambacho hakitakiwi. Kwa mfano, vigumu kupata idadi
kamili ya mashabiki wa wasanii hao, ingawa mapokeo ya kazi zao yanaweza
kumuongoza mtu kuelewa.
Kitu kimoja cha msingi ambacho wengi wanakubaliana ni kwamba Alikiba ana
uwezo mkubwa wa kuimba na mwenye sauti nzuri kuliko Diamond. Msanii
mmoja chipukizi, Ibrahim Kidugu ‘Wizzy Rapper’ katika kibao chake cha
Kote Nisikike, kwenye mojawapo ya vesi anasema “Ali ni mwanamuziki,
Nasibu Mfanyabiashara.”
Maana ya Wizzy Rapper ni kuwa Diamond anafanya biashara ya muziki, ndiyo
maana anaonekana kuwa juu ya Alikiba ambaye anafanya muziki kwa mazoea.
Katika ubora wake, Alikiba aliwahi kukutana na mkali wa R&B duniani,
R Kelly, katika projekti iliyoitwa One8, ambapo wakali nane wa Afrika
walifanya ngoma moja iliyoitwa Hands Across Africa ambao walikuwa ni
yeye, Fally Ipupa, 2Face, Amani, Movaizhaleine, 4X4, Navio na JK.
Licha ya Kiba kufika nyumbani kwa R Kelly, studio kwake, alishindwa
kutumia ushawishi wa msanii huyo mkubwa ili aweze kumsaidia kuingia
katika soko la Marekani. Mbaya zaidi, alishindwa pia kujitangaza
kimataifa kupitia Fally Ipupa na 2Face ambao ni maarufu kuliko yeye.
Ambwene Yessaya ‘AY’ alimkutanisha Diamond na Davido wa Nigeria na
akafanya naye Ngoma ya Number One Remix. Hapa kijana yule wa Tandale
hakutaka kuishia kwa msanii huyo pekee, akaingia nchini humo na kufanya
kazi na wasanii karibu wote wakubwa, wakiwemo waliofanikiwa zaidi, P
Square.
Hiyo imempa Diamond kujulikana zaidi na kumfanya kuwa mmoja wa wasanii
wakubwa Afrika, kiasi cha wengi kuhitaji kolabo naye kutoka Afrika
Kusini, Zimbabwe, Ivory Coast na kwingineko Afrika.
Alikiba haonekani kuwekeza akili yake yote katika muziki anaoufanya. Ni
kama mtu ambaye anafanya muziki kwa kujifurahisha na siyo kufikia
malengo ambayo mashabiki wake wangependa aende. Ana uwezo mkubwa nyuma
ya Mic, lakini ameshindwa kuutumia ili kuliteka soko.
Kiba anaridhika au labda niseme, mvivu. Katika uhalisia ni makosa
kumshindanisha na Diamond kwa sababu haoneshi kama ni mshindani wake.
Alipokuwa katika ziara yake Ulaya, akaitumia nafasi adimu aliyoipata
kukutana na marehemu Papa Wemba na kufanya naye wimbo.
Baada ya kuliweza soko la Afrika, Diamond anaonekana wazi kulitamani la
Ulaya na Marekani na hii ndiyo sababu ya yeye kuwa msanii anayelipwa
zaidi kuliko wote kwa sasa hapa Bongo.
Kiba hatafuti kolabo na watu wa nje kwa vile anadhani ataonekana
anamuiga mwenzake, wakati katika maisha, kuiga vitu vizuri na vya
maendeleo ni jambo la kupongezwa.
Hata hivyo, Kiba anayo nafasi ya kubadilika ili aweze kuwa mshindani wa kweli wa Diamond, vinginevyo asahau.
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!