Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi
wasikilizaji na karibuni katika kipindi kingine cha Ijue Afya yako.
Wiki iliyopita tulianza kuzungumzia tatizo la aleji au mzio, mada ambayo
leo pia tutaendelea kuijadili. Pia tutazungumzia aleji inayosababishwa
na dawa na namna ya kujikinga nayo. Tafadhalini jiungeni nami hadi
mwisho wa kipindi.
&&&&&&
Kama tulivyosema wapenzi wasikilizaji
mzio au aleji ni matokeo ya mpambano uliopitiliza kati ya kinga ya mwili
na kitu chochote ambacho kwa ujumla huwa hakina madhara kwa mwili,
inapotokea kimeingia ndani ya mwili au kimegusa sehemu fulani ya mwili.
Unachopaswa kukijua kuhusu mzio ni hali inayotokea wakati seli za mwili
wako zinapokataa kitu ambacho kwa mtu wa kawaida hakina madhara. Mzio
hujitokeza kwa alama au dalili mbalimbali na huleta matokeo yenye ishara
nyingi mwilini. Kuna aina mbili kuu za mizio, zile zinazosababishwa na
kitu ambacho kiko nje ya mwili na husababishwa na mazingira ya nje ya
mwili wako. Aina nyingine kuu ya mzio ni ile ambayo iko ndani ya mwili
wako ambayo inaweza kuletwa na kinasaba cha kurithi au na kitu kilichoko
ndani ya mwili wako.
Mzio wa ngozi au aleji inayojitokeza kwenye
ngozi ni tatizo linaloweza kukupata kutokana na mwili wako kukataa kitu
fulani, hutokana na sababu kadhaa ikiwemo hewa na hata chakula
tunachokula. Kuna vitu ambavyo huibua mzio kama vumbi katika nyumba,
mavi ya panya, manyoya ya wanyama na hewa yenye aina ya spiriti. Mzio
unaweza kukufanya uwe na ukurutu, mafua, pumu na hata kuvimba kwa mwili.
Wapo watu ambao hupata tatizo la ngozi, kuwashwa na hata kuvimba.
Katika dunia ambayo inatamba sana na teknolojia, tatizo la mzio ni kubwa
na hasa kutokana na kemikali zinazotumika katika vyakula na hata urembo
vinapotibua kemikali zinazotengeneza aleji katika mwili.
Wakati kitu
chochote kinaweza kuwa alejeni lakini kuna vitu vingine ambavyo
husababisha mzio zaidi kupita kiwango cha kawaida. Alejeni zinaweza kuwa
vumbi na mazingira yaliyochafuliwa kwa poleni (unga wa mimea na maua),
vipodozi na marashi ya kujipaka au ya kupuliza, vyakula mbalimbali kama
mayai, karanga, kemikali zinazotumika kuhifadhia vyakula na vinywaji
ambazo mtu huzila kwenye chakula au kuzinywa kwenye vinywaji hivyo. Mzio
unaweza kusababishwa na mabaki au uchafu wa kemikali kutoka viwandani,
moshi wa magari machakavu na makukuu utokao kwenye ekzosi, mwanga wa
jua, nyuzi za nguo zinazotengenezwa viwandani, baadhi ya dawa kama
penicillin na kadhalika, manyoya, sufi ya ngozi za wanyama, wadudu
mbalimbali kama mchwa na mende, manyoya ya paka na mbwa na hata harufu
inayotokana na rangi mbalimbali.
&&&&&
Wasikilizaji wapenzi mzio unaosababishwa
na dawa au drug allergy ni hali isiyo ya kawaida inayooneshwa na mfumo
wa kulinda mwili kutokana na dawa. Dawa za aina yeyote zinaweza kuleta
aleji kuanzia zinazoruhusiwa kununuliwa kwenye duka la dawa bila cheti
yaani over-the-counter drugs, zilizoandikwa na daktari au hata dawa za
mitishamba. Hata hivyo mzio husababishwa zaidi na dawa za hospitalini.
Aleji inayosababishwa na dawa huweza kuleta madhara makubwa kwa mtu, na
kuonesha dalili jumla mara moja, hali inayojulikana kama Anaphylaxis
ambayo hutishia maisha kwa kuathiri viungo kadhaa vya mwili. Mwili
unaweza kuonesha aleji za dawa za aina mbalimbali, kuanzia muwasho
kidogo kwenye ngozi hadi athari zinazoweza kusababisha madhara makubwa
mwilini. Lakini mara nyingi dalili za mzio uliosababishwa na dawa
huonekana kwenye ngozi. Kwa kawaida aleji inayosababishwa na dawa huwa
haijitokezi mara ya kwanza dawa inapotumiwa, bali pale dawa inapotumiwa
tena. Kama mzio utajitokeza mara ya kwanza mtu anapotumia dawa fulani,
kwa kawaida huwa amewahi kutumia dawa hiyo lakini bila kujua. Hii ni kwa
sababu mzio hautokei mara ya kwanza dawa inapoingia mwilini bali mara
hiyo mwili hutengeneza kingamwili au zindiko na seli za kumbukumbu za
lymphocyte kwa ajili ya dawa hiyo ambayo huchukuliwa kama kitu
kisichotakiwa na mwili au antijeni. Wakati dawa hiyo inapotumiwa tena na
kuingia mwilini seli za kingamwili huzalisha kemikali zinazoitwa
'mediator'. Mfano wa seli hizo ni Histamine ambazo athari yake kwa
viungo ni dalili ambazo hudhihirika kama aleji.
Aleji ya dawa si sawa
na athari ya dawa, inayoweza kujitokeza baada ya kula dawa ya aina
fulani, ambayo kwa kawaida huambatanishwa na maelezo ya dawa. Mzio
unaosababishwa na dawa pia ni tofauti na sumu ya dawa ambayo hutokea
pale dawa inapotumiwa kwa kiasi kikubwa. Kuna baadhi ya dawa ambazo
husababisha sana mzio kuliko nyinginezo. Dawa hizo kwanza kabisa ni
antiobiotics kama vile penicillin, tetracycline na dawa zenye sulfa
ambazo hutumika kutibu ugonjwa wa malaria. Asprini na dawa nyinginezo za
kutuliza maumivu na kupunguza uvimbe zinazojulikana kama NSAID kwa
mfano ibuprofen na indometacine. Pia dawa za kutibu saratani, dawa za
kupooza mfumo wa kulinda mwili au zinazotibu magonjwa yanayosababishwa
na hali hiyo kama vile rheumatoid fever na arthritis na krimu au lotion
aina ya corticosteroid. Nyinginezo ni dawa zinazotumiwa na watu wenye
Ukimwi na pia dawa za kutibu kifafa kama vile phenytoin au
carbamezapine. Nyinginezo ni dawa au bidhaa zinazotokana na asali ya
nyuki na pia mmea wa Echinacea ambao hutumika sana kama dawa.
Uwezekano
wa aleji kujitokeza ni mkubwa zaidi pale dawa inapotumiwa mara nyingi,
inapopakwa juu ya ngozi au kudungwa mwilini kwa sindano, kuliko wakati
inaponywewa kupitia mdomo. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, mzio
wa dawa humaanisha kuwa mwili umekataa dawa fulani au haupatani nayo.
&&&&&&
Dalili za aleji inayosababishwa na dawa
kwa kawaida hutokea katika kipindi cha saa moja baada ya kutumiwa dawa.
Mara chache aleji huweza kutokea pia baada ya masaa, siku au wiki
kadhaa. Miongoni mwa dalili za mzio wa dawa ni vipele vya ngozi,
muwasho, kuvimba, macho kutoa machozi na ngozi kubadilika rangi. Dalili
nyinginezo za aleji ya dawa ni homa, kuvimba, kubanwa na pumzi, makamasi
na kupumua kwa kutoa sauti kama mtu anayepiga filimbi hali
inayojulikama kitaalamu kama wheezing.
Mara chache mzio wa dawa
huweza kusababisha madhara makubwa kwa mtu ambapo mwili huonesha dalili
ya jumla inayohatarisha maisha ijulikanayo kama Anaphylaxis ambayo
hukwamisha utendaji wa mfumo wa mwili. Viashiria vya hali hiyo ni
kubwanwa njia ya hewa na koo, suala linalopelekea kushindwa kupumua.
Kichefuchefu au maumivu ya tumbo yasiyo ya kawaida, kuharisha au
kutapika, kizunguzungu au kuhisi kichwa chepesi, mwili kudhoofika na
mapigo ya moyo kwenda mbio. Pia mwenye hali hiyo presha yake hushuka,
huwa na dalili za kifafa na kupoteza fahamu.
Vilevile kuna matatizo
ambayo yanaweza kujitokeza baada ya siku au wiki kadhaa baada ya kutumia
dawa, ambayo yanaweza kubakia kwa muda mrefu hata baada ya kuacha
kutumia dawa. Matatizo hayo ni ugonjwa wa Serum ambao husabisha homa,
maumivu ya viungo, vipele, kuvimba na kichefuchefu. Tatizo jingine ni
ukosefu wa damu ambapo chembe nyekundu za damu hupungua na pia kuvimba
figo na kutokewa na vipele vinavyoambatana na matatizo katika seli
nyeupe za damu.
&&&&&&
Mpenzi msikilizaji iwapo utatumia dawa
na kwa bahati mbaya zikakuletea aleji unapaswa kumuona daktari mara moja
au kwenda hospitali haraka ili kupata matibabu na kuondoa aleji. Iwapo
utapata dalili zinazoashiria Anaphylaxis kama tulivyoeleza kabla
unapaswa kuomba haraka msaada wa kitiba ili kuokoa maisha. Pia unapaswa
kuacha kutumia dawa iliyokusababishia dalili kali za mzio.
Na kufikia
hapo wapenzi wasikilizaji hatuna la ziada, natumaini mmefaidika vya
kutosha. Tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa na tusisahau
kuzitunza afya zetu!
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!