SIYO kwamba sijui faida za maziwa ya mama kwa mtoto.
Nafahamu wazi kwamba, maziwa ya mama ndiyo chakula pekee
kinachompatia mtoto virutubisho (viini lishe) vyote muhimu anavyohitaji
kwa uwiano ulio sahihi kwa ajili ya ukuaji na maendeleo yake. Nafahamu
kabisa kwamba, maziwa ya mama humpatia mtoto kinga dhidi ya maradhi
mbalimbali kama vile kuharisha, magonjwa ya njia ya hewa na masikio.
Lakini pia humwezesha mtoto kukua kimwili na kiakili kikamilifu. Zaidi
ya yote, ninazo taarifa za kitaalamu kwamba, unyonyeshaji huleta
uhusiano mzuri na wa karibu kati ya mama na mtoto.
Kupitia machapisho mbalimbali na hata mafunzo ya moja kwa moja ya
wataalamu, naelewa kwamba watoto walionyonya maziwa ya mama huwa na
mwenendo mzuri pamoja na akili ukilinganisha na wale wasionyonya maziwa
ya mama. Hata kwenye kliniki ya ujauzito, wauguzi na wakunga
wamenielewesha kuwa maziwa ya mama humeng’enywa (huyeyushwa) kwa urahisi
tumboni mwa mtoto na hivyo kutumiwa na mwili kwa ufanisi.
Ikiachwa faida kwa mtoto, ninayo maarifa kwamba unyonyeshaji pia
husaidia kulinda afya ya mama. Nimesoma hata kwenye machapisho ya afya
kwamba, mama anaponyonyesha mara baada ya kujifungua husaidia tumbo la
uzazi kurudi katika hali ya kawaida mapema. Pia husaidia kupunguza damu
kutoka hivyo kuzuia upungufu wa wekundu wa damu (upungufu wa damu).
Jambo lingine ambalo mimi na akina mama wengi tunalifahamu hata bila
msaada wa wataalamu, ni kwamba unyonyeshaji hupunguza uwezekano wa
kupata ujauzito.
Ni endapo mama atamnyonyesha mtoto katika miezi sita ya maziwa yake
tu, mara nyingi kwa siku na pia kama hajapata hedhi; Mafunzo mengine
ambayo nimeyapata kwa njia tofauti, ni kwamba, kumnyonyesha mtoto
hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya mfuko wa uzazi, na matiti.
Pamoja na faida hizo kwa mama na mtoto, baada ya kujifungua watoto
pacha, sikufanikisha kuwanyonyesha kama ambavyo kanuni zinaelekeza.
Sikuwa na namna ya kuwalazimisha wanangu wanyonye; kwani walinigomea
wakiwa na miezi sita.
Hawakutaka kuendelea kunyonya maziwa yangu. Tatizo lilianza wakiwa na
miezi mitano. Walinogewa na maziwa ya kopo. Hii ni kwa sababu baada ya
kumaliza likizo yangu ya uzazi ya miezi mitatu na kuanza kazi,
ilinilazimu kuwaanzishia maziwa mbadala. Kutokana na msongamano wa
barabarani katika jiji la Dar es Salaam, nilikuwa nikifika jioni
nyumbani na kukuta wameshakunywa maziwa ya kopo. Kwa hiyo walizoea
maziwa hayo ya kopo ambayo naamini yaliwafanya wapoteze hamu ya maziwa
yangu.
Isitoshe, nionavyo, maziwa ya kwenye chupa yalitoka kwa wingi
ikilinganishwa na ya mama ambayo yalitoka kidogo. Hayakuwatosheleza
watoto hao pacha. Sikuwa na njia nyingine ya kuwatosheleza watoto zaidi
ya kuingia mfukoni kwa ajili ya kununua maziwa ya kopo na vyakula
vingine vya kuwawesha kuwaongezea lishe mwilini. Lakini pia nakumbuka,
ile kanuni ya kwamba, mtoto aanze kunyonya maziwa ya mama mara tu baada
ya kuzaliwa (katika saa moja ya kwanza), kwangu haikufanyika.
Kuchelewa kunyonyesha baada ya kujifungua
Baada ya kujifungua kwa operesheni, ilinichukua saa nyingi kabla ya
watoto kuletwa niwanyonyeshe maziwa ya kwanza. Lakini haikuwezekana
kutokana na kwamba, maziwa yalikuwa hayatoki. Tatizo la kuchelewa kuanza
kuwanyonyesha kwa wakati watoto mara nyingi huwapata wazazi
wanaojifungua kwa operesheni, lakini wakati mwingine huchangiwa na
wauguzi wasio makini.
Kwa ujumla, sikutimiza maelekezo ya kitaalamu yanayotaka mtoto
asipewe kitu kingine chochote hata maji, isipokuwa maziwa ya mama mpaka
afikie umri wa miezi sita. Kwani wanangu walianza kupewa uji na maziwa
ya kopo wakiwa na umri wa miezi mitatu. Hiyo ni simulizi ya Shukuru
Amani (siyo jina halisi) alipofanya mahojiano na waandishi wa makala
haya. Shukuru anawakilisha kilio cha wanawake wengi ambao mazingira,
hususani ya ajira, yamewafanya washindwe kuwanyonyesha watoto wao katika
muda unaotakiwa.
Hakuna ubishi kwamba mazingira ya ajira ndiyo yamechangia watoto wake
pacha kunyonya kwa muda mfupi kabla ya kukataa wenyewe wakiwa na umri
wa miezi sita. Ingawa wapo akina mama wengine ambao inadaiwa kutokana na
sababu binafsi, hukataa kuwanyonyesha watoto wao, kwa Shukuru ni
tofauti. Alitamani kuwanyonyesha watoto wake kila siku na kwa muda
mrefu.
Ukamuaji maziwa
Hata hivyo, laiti Shukuru angezingatia utaratibu wa kukamua maziwa na
kuyaacha nyumbani kwa ajili ya kuwalisha watoto wake, pengine
asingekumbana na tatizo la watoto kukataa maziwa ya mama, maziwa ambayo
yangekuwa mchango mkubwa katika afya zao, mintarafu suala zima la
kujenga akili zao na ukuaji wa mwili. Wataalamu wanasema kwamba ukamuaji
maziwa ni njia ambayo inaweza kuwasaidia akinamama walioko maofisini au
kwenye shughuli za biashara kuwahakikishia watoto wao maziwa yao pale
wanapokuwa hawako nyumbani.
Wanasema maziwa ya mama yakikamuliwa na kuwekwa kwenye chombo kisafi
yanaweza kukaa kwa muda wa saa 8 bila kuharibika na yakiwekwa kwenye
jokofu huweza kukaa zaidi ya saa 36. Hakuna utafiti umefanyika kwa
watoto pacha wa Shukuru kujua kama wana tatizo la udumavu au la, lakini
kutonyonyesha vizuri watoto hadi kufikia umri wa miaka miwili au zaidi
kunatajwa pia kuwa chanzo cha udumavu.
Udumavu ni hali ya watoto kutokua kimwili na kiakili hadi kiwango
kinachotakiwa kutokana na lishe duni yakiwemo maziwa ya mama na hili
huanzia wanapokuwa tumboni mwa mama zao. Kwa mujibu wa Jukwaa la Lishe
nchini (Panita), udumavu mara nyingi hutokea ndani ya siku 1,000 za
mtoto zinazohesabiwa tangu mimba kutungwa hadi mtoto anapofikisha umri
wa miaka miwili kamili.
“Siku hizi 1,000 zikizingatiwa na wazazi kwa maana ya lishe bora kwa
mama na mtoto akishazaliwa kwa kumnyonyesha ipasavyo hadi kuadhimisha
miaka miwili ya kuzaliwa kwake, hupunguza pia uwezekano wa magonjwa ya
muda mrefu na mzio (allergy),” anasema Jane Msagati, Mtaalamu wa Lishe
wa Panita. Anasema mtoto akishakuwa na udumavu, ni tatizo
lisilorekebishika maisha yake yote na kwamba hata kama ukimwangalia kwa
umbo ukaona hana tofauti na wengine, lakini huwa nyuma kwa kila kitu
kulinganisha wenzake hususani kwenye masomo darasani.
Jane anatoa takwimu za mwaka jana zinazoonesha kwamba watoto milioni
2.5 wa Tanzania, sawa na asilimia 34 ya watoto wote walipata udumavu.
Takwimu zingine zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto zinaonesha kwamba Mkoa wa Rukwa, ndio unaoongoza
kwa udumavu, ukiwa na asilimia 56.6 ya watoto wenye tatizo hilo
ukifuatiwa na Ruvuma yenye asilimia 44.4, Kagera yenye asilimia 41.7 na
Iringa yenye asilimia 41.6.
Sababu zaidi watoto kukataa kunyonya
Kama tulivyoona kwa kisa cha Shukuru kwamba watoto wanaweza kukataa
kunyonya kutokana na mama kuchelewa kuwanyonyesha kutokana na ajira,
mtoto anaweza pia kukataa maziwa kutokana na kile anachokula mama na
kusababisha maziwa kuwa na harufu au ladha tofauti. Jane wa Panita
anasema endapo mama atakuwa anakunywa pombe wakati ananyonyesha, kuna
uwezekano wa maziwa kuwa na harufu ya pombe kiasi cha kumfanya mtoto
kuyakataa.
Anasema maziwa yanaweza pia kuwa na harufu kutegemea dawa alizotumia
mama kutibu maradhi fulani. “Ndio maana mama anayenyonyesha anapopata
maradhi, lazima dawa anazotakiwa kunywa ziwe ambazo zinaruhusiwa kwa
mama anayenyonyesha vingine zinaweza kumwathiri mtoto ikiwemo hiyo ya
kusababisha maziwa yake kuwa na harufu au ladha itakayomfanya
ayachukie,” anasema Jane.
Machapisho kadhaa yanaonesha kwamba kama mama hamweki vizuri mtoto
wakati wa kunyonya kinaweza kuwa pia chanzo cha mtoto kukataa kunyonya.
Kusaidia akinana mama walio kwenye ajira Kama tulivyosikia kisa cha
Shukuru, ajira ilichangia sana kuwafanya wanawe kukataa kunyonya. Ili
kuwasaidia akina mama kama Shukuru kumekuwa na mapendekezo ya aina
mbili, moja likiwa ni kuongeza muda wa likizo ya uzazi.
Wakati dunia inaadhimisha wiki ya unyonyeshaji watoto , umefika
wakati sheria za kazi ziangaliwe; ikiwezekana, mama apate likizo ya
uzazi kwa zaidi ya miezi sita au hata mwaka. Ingawa kwa sasa akina mama
wanaonyonyesha huruhusiwa kuondoka kazini mapema, lakini kwa jiji kama
la Dar es Salaam ambalo lina tatizo kubwa la usafiri na foleni, wengi
wanalalamika kwamba bado wanachelewa kufika nyumbani na hivyo
kutowanyonyesha watoto wao kwa muda mwafaka.
Pendekezo lingine linalotolewa ni waajiri kutenga vyumba maalumu kwa
ajili ya kunyonyeshea, ambavyo vitawawezesha watumishi waliojifungua
kuja na watoto wao mafisini baada ya kumalizika kwa likizo ya uzazi.
Katika pendekezo hili ambalo baadhi ya ofisi katika nchi jirani ya
Kenya zimeshalifanyia kazi, vyumba vinavyotengwa vinatakiwa kuwa na
vifaa maalum kwa ajili ya watoto kama vile vitanda vya watoto, majokofu,
jiko na vifaa vya kucheza. Sambamba na hilo, waajiri wanatakiwa pia
kuajiri yaya mmoja au zaidi kwa ajili ya kulea watoto wa watumishi. Ni
kwa njia hiyo mama anaweza akawa mara kwa mara anatoka kwenda
kunyonyesha mtoto wake katika mazingira ya kazini na kurejea kuendelea
kuchapa kazi.
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!