WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,
amesema Serikali inataka kuona Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ikizaliwa
upya na kutoa ushindani wa hali ya juu katika soko la mawasiliano
nchini.
Alisema hayo jana, Dar es Salaam alipozungumza na wafanyakazi wa
kampuni hiyo na kuongeza kuwa Serikali imefanya mengi kuiwezesha kuwepo
na kuendelea kuhudumia Watanzania, huku akisisitiza kuwa siku chache
zilizopita, kampuni ya Bharti Airtel ililipwa Sh bilioni 14.9 na
kuachana rasmi na kampuni hiyo.
“Ndugu wafanyakazi, sasa ni wakati wa kufanya kazi, hatuna tena muda
wa kupoteza, muda tulionao ni wa kuwajibika, kuwatumikia wananchi,
Serikali inafanya kila jitihada kuwezesha na tunachotaka kwenu ni
uadilifu, hatuna nafasi kwa wabadhirifu, wavivu na wanaovujisha siri za
kampuni kwa washindani,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema ni lazima kubadilika na kufanya kazi kwa juhudi kubwa
wananchi waridhike huku akikemea tabia ya vyama vya wafanyakazi kutumia
muda mwingi kulumbana na kuendesha migogoro isiyo na tija kwao na
kampuni na badala yake wafanye kazi kwa bidii kila mmoja akitimiza
wajibu.
Awali akitoa taarifa fupi kwa Waziri, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk
Kamugisha Kazaura, alisema kampuni hiyo inashukuru mchango mkubwa wa
Serikali kuiwezesha kuendelea kutimiza wajibu wake.
“Kuondoka kwa kampuni ya Bharti Airtel ndani ya TTCL, Serikali
kuisamehe madeni ya Sh bilioni 100, kuipatia masafa ya mawasiliano na
kibali cha kutumia rasilimali zake kama dhamana ili kupata fedha za
kufanikisha mipango na mikakati yake ya kibiashara,” alisema.
Aidha Dk Kazaura alisema, kutokana na mchango huo mkubwa wa Serikali,
kampuni hiyo imeongeza ufanisi wake ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa
huduma za 4G LTE ambazo hadi sasa zimesambaa katika maeneo 33 jijini Dar
es Salaam na mpango ni kufikia mikoa mingine mitatu ifikapo mapema
mwakani.
Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Profesa Tolly Mbwete alisema, kampuni hiyo imejipanga kikamilifu kutoa huduma bora.
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!