WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema Serikali
inasubiri Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) naTume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC) zimalize majadiliano ili mchakato wa kuipigia kura ya maoni Katiba
Inayopendekezwa ufanyike.
Waziri Mwakyembe alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana
alipokutana na uongozi wa Kikosi cha Kupambana na Haki za Mirathi
(Kikuhami ) kilichoko chini ya Chama cha Wanawake katika Sheria na
Maendeleo Afrika (WiLDAF).
Alisema kura hiyo ya maoni ingekuwa imeshafanyika lakini Tume za
Uchaguzi ziliona ni bora iahirishwe kwanza ili kupisha nchi kukamilisha
Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Alisema kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu kunatoa fursa kwa Serikali
kuendelea na mpango wake wa kuendesha kura ya maoni juu ya Katiba
Inayopendekezwa ili kupata Katiba Mpya ya Tanzania.
Aliongeza kuwa Katiba Inayopendekezwa ina vitu vingi sana ambavyo
vitasaidia upatikanaji wa haki za wanawake na kuondoa uonevu dhidi yao
na hivyo kufanikisha harakati ambazo wadau mbalimbali wanawake nchini
wamekuwa wakizipigania na hivyo kukamilika wakati Katiba Mpya
itakapokuwa imepatikana.
Aidha Waziri aliutaka uongozi huo wa Kikuhami kupitia WiLDAF
kuwasilisha wizarani mapendekezo yao juu ya mabadiliko ya sheria
mbalimbali za mirathi nchini wanazoziona zinawakandamiza wanawake ili
ziweze kufanyiwa marekebisho na ziendane na wakati uliopo.
Kikuhami chini ya uongozi wa Thabita Siwale ulimuomba Waziri
Mwakyembe kuangalia uwezekano wa kuondoa sheria zinazowakandamiza
wanawake hasa zile za mirathi.
Share And Comment Bellow On What You Think About This Post!!!
Comments
Post a Comment
Welcome.......
What are you thinking of....!!